Thursday 4 October 2012

Zitto apeleka hoja bungeni kutaka uchunguzi walioficha mabilioni nje

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ameiandikia barua Ofisi ya Bunge kuitaarifu nia yake ya kuwasilisha hoja binafsi katika Mkutano wa 11 wa Bunge kuliomba liazimie Serikali iwasiliane na taasisi za kimataifa, hasa benki kusaidia kurejeshwa nchini fedha zote haramu ambazo zimefichwa na Watanzania katika benki za nchini Switzerland na kwingineko duniani.
Taarifa zilizopatikana jana kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni zimeeleza kuwa Zitto anaomba Serikali ifanye hivyo kwa Benki ya Dunia kupitia taasisi yake ya Stolen Asset Recovery Initiative, kutekeleza jukumu hilo.
Taarifa hizo zimeeleza kuwa katika barua hiyo Zitto anatumia kifungu cha kanuni za bunge namba 55 (1) na (2), na hoja yake itaainisha fedha ambazo Benki ya Taifa ya Switzerland ilitangaza kwamba Watanzania wamezihifadhi, ambazo ni Sh297 bilioni.
Barua hiyo imeainisha kuwa fedha hizo ni sawa na Dola za Marekani 186 milioni na Zitto amebainisha kuwa hoja yake hiyo itaainisha namna na njia ambazo zilitumika kutorosha fedha hizo kwenda katika benki hiyo na nyingine za nje.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah alikataa kuthibitisha kupokea barua hiyo badala yake alieleza kuwa hilo ni suala la kiofisi.
"Ni suala la ndani la ofisi, siwezi kueleza kama ni kweli nimepokea au la, isipokuwa suala hilo linafahamika na ofisi ya Bunge ililipokea alipoliwasilisha bungeni hivyo linafanyiwa kazi," alisema Kashillilah.
Mapema mwaka huu, baadhi ya vyombo vya habari likiwamo gazeti hili, vilifichua kuwapo kwa fedha zilizofichwa nchini Uswisi na baadaye ilibainika kwamba fedha hizo ni mali ya Watanzania 27 wakiwamo wanasiasa na wafanyabiashara.
Gazeti hili pia lilibaini kwamba mmoja wa walioficha fedha hizo anamiliki Dola za Marekani milioni 56 (sawa na Sh89.6 bilioni).
Katika uchunguzi wake, Mwananchi limebaini pia kuwa kiasi cha fedha kilichothibitishwa kumilikiwa na Watanzania hao ni jumla ya Dola za Marekani 186 milioni (takriban Sh300 bilioni) kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1600 kwa Dola ya Marekani.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa mbali na kigogo anayemiliki Sh90 bilioni, wapo wengine wanne, ambapo anayefuatia anamiliki Dola 30 milioni (Sh48 bilioni), mwingine Dola 20 milioni (Sh32 bilioni) na wengine wawili kila mmoja anamiliki Dola 10 milioni (Sh16 bilioni).
Kwa kuangalia fedha hizo ni dhahiri kwamba vigogo watano tu kati ya kundi la Watanzania 27, wanamiliki Dola 126 milioni (Sh201.6 bilioni) sawa na asilimia 67.74 ya fedha hizo, wakati wengine 22 waliobaki wanamiliki Dola 60 milioni (Sh96 bilioni) sawa na asilimia 32.25.
Habari hizo zilikuwa zikinukuu taarifa ya Benki Kuu ya Uswisi iliyoitoa na kuonyesha kuwapo kwa kiasi cha Sh315.5 bilioni zilizotoroshwa Tanzania na kufichwa nchini humo na vigogo ambao ni wanasiasa pamoja na wafanyabiashara.
Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU