Friday, 5 October 2012

MBUNGE WA MUSOMA MJINI, VICENT NYERERE (CHADEMA) AMETOA RUNIGA KWA WAFANYABIASHARA WA SOKO KUU LA MUSOMA ILI WAWEZE KUPATA HABARI WAWAPO KAZINI

MBUNGE wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (CHADEMA), amekabidhi runinga 10 kwa wafanyabiashara wa soko kuu la Musoma mkoani Mara. Mbunge huyo alikabidhi runinga hizo jana, zenye thamani ya Sh milioni 9, katika eneo la ndani ya soko hilo lenye wafanyabiashara wengi.

Nyerere alisema kuwa, wafanyabiashara wa sokoni wamekuwa wakikosa haki ya kupata habari za uhakika, kutokana na kushinda kutwa nzima sokoni.

“Wafanyabiashara wa sokoni ni watu wa kuhangaika, hawana televisheni katika maeneo yao ya kazi na wanaporudi nyumbani, hupata habari za kusikia kwa watu,” alisema.

Amesema runinga hizo zitawasaidia kupata habari za mambo mbalimbali yanayoendelea nchini, ikiwa ni pamoja na uendeshwaji wa vikao vya Bunge.

“Wanapitwa na mambo mengi, vikao vya Bunge huanza asubuhi muda ambao wafanyabiashara hawa wapo sokoni, wanakosa haki ya kupata habari,” alisema.

Akipokea runinga hizo kwa niaba ya wafanyabiashara, Ofisa Biashara wa Manispaa ya Musoma, God Machumu, alimpongeza mbunge huyo kwa kutimiza ahadi yake kwa wananchi.

Mbali ya kupokea runinga hizo, wafanyabiashara hao walimweleza mbunge huyo changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika soko hilo.

Miongoni mwa changamoto hizo, ni pamoja na usumbufu nyakati za masika, kutokana na soko hilo kujaa maji, hali inayosababishwa na soko hilo kukosa mitaro ya maji.

Tatizo la ulinzi katika soko hilo limeelezwa kuwa, kikwazo katika maendeleo ya wafanyabiashara hao kwa madai kuwa, wamekuwa wakiibiwa mali zao kutokana na kutokuwepo kwa ulinzi wa kuaminika.

No comments:

Post a Comment

Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU