Wednesday 3 October 2012

Rufani Ya Lema Yatikisa Arusha


Video Rufaa ya Godbless Lema
 
Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema akiwahutubia wafuasi wake baada ya Jaji MKuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman kuahirisha kesi ya rufaa ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema.Picha Zote na Jackson Odoyo Mussa Juma, Arusha MAWAKILI wanaomtetea aliyekuwa Mbunge wa Arusha, Godbless Lema wamedai mbele ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuwa mteja wao yuko huru kwa kuwa mahakama haikutengua ubunge wake.Katika kesi hiyo, Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande anawaongoza wenzake wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati na Natalia Kimaro kusikiliza maombi ya rufani hiyo, inayopinga Lema kuvuliwa ubunge.

Mawakili hao wa Lema jana walitoa hoja ya kupinga hukumu hiyo kufuatia mabishano baina yao na upande wa utetezi kwa maelezo kuwa taratibu za ufunguaji wa rufaa hiyo zimekosewa. Awali wakili Alute Mughwai aliiomba mahakama hiyo kutupilia mbali rufani hiyo kwa kile alichoeleza kuwa ina upungufu mwingi wa kisheria na kikanuni. Wakili huyo alitaja baadhi ya kasoro za rufani hiyo kuwa ni hati ya kukaza hukumu (tuzo) ambayo imewasilishwa mahakamani hapo kutokuwa na mhuri wa Jaji Gabriel Rwakibarila aliyetoa hukumu ya kesi hiyo.
Alidai kuwa katika rufani hiyo pia kuna upungufu kuhusu tarehe za kuwasilishwa kwa rufani, pia baadhi ya vifungu vimekosewa.Wakili Mughwai alitoa kumbukumbu ya kesi kadhaa ambazo mahakama ya rufani ilizitupa baada ya kukosa hadhi ya kisheria kusikilizwa.

“Mawakili wa Lema walipaswa kabla ya kuwasilisha mahakamani rufani yao, kujiridhisha kama kuna upungufu katika nyaraka ambazo wanawasilisha mahakamani.”Alisema kubwa katika makosa ambayo amebaini katika rufani hiyo ni kuwasilishwa bila kuwekwa mhuri hati ya kukaza hukumu (tuzo) iliyotolewa na Jaji aliyetoa hukumu katika kesi ya awali.“Hapa nani ambaye anajua sahihi ya Jaji? Alihoji. Hawa mawakili walipaswa kushinikiza kuwekwa mhuri wa mahakama katika hukumu hiyo ili kuthibitisha uhalali wake,” alisema Alute. Hata hiyo, wakili huyo alisema badala yake, mawakili hao waliwasilisha mahakamani rufani hiyo ndani ya siku 29 tu baada ya hukumu, badala ya siku 60 ambazo walipewa.

Kwa kuwasilisha mahakama ya rufani, hukumu ambayo bado haina mhuri wa Jaji ni ukiukwaji wa kanuni na taratibu za mahakama.”Mughwai alidai kuwa katika mazingira ya sasa hakuna cha kurekebishwa katika rufani hiyo, badala yake itupwe na kuwataka wakata rufani kulipa gharama zote za kesi. Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na mawakili wa Lema ambao ni Tundu Lissu na Method Kimomogoro, ambao walidai kuwa hawakuwa na mamlaka ya kumlazimisha Jaji Rwakibarila kuweka mhuri.

Lissu alidai "Kama inaonekana sasa kuwa ni batili, basi hata uamuzi wa kumvua ubunge Lema ni batili," alisema. Wakili Kimomogoro Kwa upande wake, Wakili Kimomogoro alisema kisheria kasoro hizo ya mhuri wa mahakama na tarehe, haziwezi kusababisha rufani hiyo kutupwa kwani haziathiri madai ya msingi katika rufani.

Alidai kesi hiyo ya Lema ilikuwa ya kipekee kwani mara tu baada ya hukumu kutolewa faili lilipelekwa jijini Dar es Salaam na maombi ya nyaraka kadhaa za kesi hiyo yalitumwa kutoka Dar es Salaam.“Katika mazingira kama haya hatuwezi kuepuka makosa ya kibinadamu ambayo yanatambulika kisheria,” alidai Kimomogoro. Aliongeza kuwa katika hoja hiyo, waliandika kifugu namba 114 badala ya 113 kimakosa ya kiuchapaji, lakini hakipotoshi kitu chochote kwani kifungu hicho hakipo. Wakili Kimomogoro alisema wakili mwenzake, Mughwai ameshindwa kuzungumzia uamuzi ya kesi ambazo, hazikufutwa kutokana na kuwa na upungufu mdogo wa aina hiyo ambao kimsingi hauathiri rufani. Hata hivyo, alisema kama wakili huyo alibaini makosa hayo, katika uwasilishaji wa hoja zake, alipaswa pia kurekebisha kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2009 ya mahakama. Kimomogoro pia aliwasilisha mahakamani hoja kadhaa za kisheria na uamuzi ya Mahakama ya Rufani za ndani na nje ya nchi, ambazo hazikutupilia mbali rufani ambazo zilikuwa na upungufu mdogo, kwani lengo la mahakama hizo ni kutafuta haki.
“Siyo kila kasoro au usumbufu kwenye hukumu unaweza kusababisha kutupwa rufani kwani kasoro zote zilizotajwa ni za makosa na uchapaji na nyingine ni za kiutaratibu tu,” alisema. Alifafanua kuwa makosa ambayo yanaweza kusababisha rufani kutupwa ni kama aina namba ya kesi, majina na wadhifa wa wadau katika shauri husika, mambo yanayolalamikiwa na mahakama imeamua nini.

Wakili huyo alifafanua kuwa jambo la kukosekana mhuri wa mahakama wa Jaji siyo kubwa na kusababisha kutupwa rufani kwani hakuna ambaye anapinga hukumu iliyowasilishwa mahakamani. Kwa upande wake, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Vitalis Timoth alisema anaunga mkono hoja za mawakili wa Lema, kuwa pingamizi ya wakili Mughwai haina msingi wa kisheria.

Alisema hati ya kukaza hukumu (Tuzo) inatolewa chini ya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai na siyo chini ya sheria ya masijala za mahakama. Alisema siyo kazi ya jaji aliyetoa hukumu, kuweka mhuri hukumu yake bali hiyo ni kazi ya msajili wa mahakama na masijala za mahakama.

Kama hati ya kukaza hukumu ina matatizo anayepaswa kulaumiwa siyo mawakili bali ni mahakama ambayo ndiyo ilikuwa na mamlaka ya kuweka mhuri,” alisema. Alidai kuwa pingamizi ya awali ya rufani inapaswa kuwa na sifa mbili, kwanza iwe na suala la kisheria na pili iendane na kesi ya msingi.“Katika hoja za wakili Mughwai ni wazi inathibitika pingamizi hili halina matakwa ya kisheria kwani hata kama ikipitwa siyo kuwa itazuia kurejeshwa tena na kusikilizwa kwa rufani ya msingi.”Alidai ni busara kuacha kuwa na pingamizi ambazo zinaongeza gharama za kesi na muda wa kusikiliza.

Ushauri wangu kila shauri liamuliwe kwa mazingira yake na uamuzi wa sasa uzingatie mahakama katika kutenda haki,” aliongeza. Alidai kwamba kutupwa kwa hoja ya kutaka waomba rufani wachapwe mijeledi kwani kazi ya mahakama siyo kuchapa watu bali ni kutoa haki.“Tunashauri kusikilizwa rufani kwa kuzingatia sheria na ushahidi,” alisema. Jopo la Majaji Baada ya kutolewa kwa hoja za pande zote za mawakili, Jaji Chande na Jaji Massati waliwauliza maswali kadhaa mawakili hao na kujieleza na baadaye Jaji Chande alitangaza kuahirishwa kwa kesi hiyo hadi hapo itakapotangazwa. Jaji Chande alisema vikao vya Mahakama ya Rufani Kanda ya Arusha vimemalizika jana, hivyo uamuzi wa kutupwa kwa pingamizi la rufani hiyo au la utatolewa siku itakayopangwa na mahakama.

Baada ya uamuzi huo umati wa wafuasi wa Chadema, uliokuwa ndani na nje ya mahakama ulianza kuimba nyimbo mbalimbali kama vile Lema Jembe na bila Lema patachimbika. Katika hatua ya kuepuka vurugu, Lema alizungumza na wafuasi hao nje ya mahakama na kuwataka kuondoka kwa amani kwenda katika ofisi ya Chadema iliyopo Ngarenaro kwa amani bila vurugu.

Warufaniwa katika kesi hiyo ni makada wa CCM, Happy Kivuyo, Mussa Mkanga na Agnes Mollel ambao walishinda kesi ambayo hukumu yake ilimvua ubunge Lema Aprili 4, mwaka huu.


 Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari

No comments:

Post a Comment

Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU