Mtei alisema amekuwa
akimshauri Zitto mara kwa mara kuhusu hatua yake hiyo akimtaka kuwaunganisha
wana Chadema na siyo kuwagawa au kuwavuruga.
Kauli hiyo ya Mtei imekuja
siku chache baada ya mbunge huyo kutangaza kwamba hana mpango wa kugombea ubunge
mwaka 2015, badala yake anajipanga kuwania urais.
“Hakuna shida kuonyesha
hisia, lakini unatengeneza mzozo mkubwa sana ukitangaza sasa. Mimi
nimeshamshauri sana Zitto, ahakikishe anakiunganisha chama na siyo kukigawa wala
kukivuruga,” alisema Mtei.
Mtei alisema hatua ya
mbunge huyo kutangaza kutogombea tena ubunge na badala yake kujipanga kuwania
urais mwaka 2015 umekuja mapema mno na kuonya kuwa itaibua mzozo ndani ya
Chadema.
Mtei ambaye aliwahi kuwa
Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu enzi za utawala wa Mwalimu Julius
Nyerere, alisema kwamba wakati mwafaka ukiwadia, Chadema kitaamua ni nani mwenye
sifa za kugombea urais akisema kina utaratibu wake wa kuwapata wagombea
mbalimbali wa uongozi.
Alisisitiza kwamba siyo
vibaya kwa Zitto kuonyesha hisia zake, lakini akasema kuwa ndani ya Chadema kwa
sasa, kuna watu mbalimbali wanaopenda kuwania urais, lakini
hawajatangaza.
“Dk Slaa (Willbrod)
anataka, Freeman (Mbowe) anataka, Zitto anataka, hata mimi huenda nikataka
kugombea. Hapa hakuna upendeleo, sifa ndizo zitakazoamua,” alisema.
Huku akimwagia sifa
mbalimbali Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini, Mtei alisema kwa upande mwingine,
Katiba ya Tanzania kwa sasa, inamnyima Zitto sifa za kuwania urais mwaka 2015
kwa kuwa hadi kufikia mwaka huo atakuwa amefikisha miaka 38, huku Katiba
ikielekeza kuwa mgombea urais anatakiwa awe na miaka isiyopungua
40.
Alipoulizwa ya kwamba
endapo uchaguzi mkuu ujao utafanyika huku Watanzania wakiwa na Katiba Mpya
iliyopunguza umri wa kuwania urais, Mtei alisema endapo mbunge huyo atapambana
kuhakikisha umri huo unapunguzwa, basi atakuwa ni mbinafsi wa
kupindukia.
“Kama yeye akichukua hatua
ya kupambana ili Katiba ibadilishwe kwa kuwa anataka kuwania urais, basi
itaonekana ni mtu wa ajabu sana; ni mtu mbinafsi na siyo vizuri.”
Zitto
apinga
Akizungumzia kauli hiyo ya Mtei, Zitto alisema: “Demokrasia haileti mizozo kwenye vyama vya siasa hata siku moja, bali humaliza mizozo. Udikteta, kuminya fikra huru na mawazo huru, ndivyo huleta mizozo kwenye vyama vya siasa.”
Akizungumzia kauli hiyo ya Mtei, Zitto alisema: “Demokrasia haileti mizozo kwenye vyama vya siasa hata siku moja, bali humaliza mizozo. Udikteta, kuminya fikra huru na mawazo huru, ndivyo huleta mizozo kwenye vyama vya siasa.”
Alisema ni muhimu wazee
wakawaacha vijana wawe huru kusema wanachofikiri kwa kuwa uhuru wa fikra na
mawazo ni moja ya haki za msingi na moja ya nguzo za demokrasia.
“Namheshimu Mtei kama mmoja
wa waasisi na mwenyekiti mwanzilishi wa chama. Chama chetu kimekua na kina uwezo
wa kuhimili demokrasia ya ndani,” alisema Zitto akiongeza kuwa miaka 20 tangu
kuanzishwa kwa vyama vingi, nchi inastahili kuimarisha vyama
kidemokrasia.
“Ninarudia, nitaomba
kupeperusha bendera ya chama changu kwenye uchaguzi wa urais mwaka 2015. Naamini
kwamba ninaweza kuwezesha chama chetu kushinda na kuongoza dola na Chadema kutoa
rais wakati baadhi ya waasisi wetu wakiwa hai na kuona vijana wao tunavyobadili
maisha ya Watanzania na kutimiza ndoto zao,” alisema Zitto.
Alisema ana uwezo, uadilifu
na uzalendo wa kutosha kuwa Amiri Jeshi Mkuu na kuunganisha Watanzania kuwa
wamoja bila kujali rika, dini wala makabila yao... “Nimejiandaa kisaikolojia
kukabili changamoto za ufukara wa nchi yetu.”
Septemba 26, mwaka huu
Zitto alitangaza nia yake hiyo ya kuwania urais mwaka 2015, alipozungumza na
wananchi katika mjadala ulioandaliwa na asasi ya kiraia ya Meza ya Duara
uliofanyika maeneo ya Soko la Mwanga, mjini Kigoma na kuhudhuriwa na watu zaidi
ya 200. Miongoni mwa maswali hayo lilihusu tetesi kwamba anataka kugombea urais
katika uchaguzi ujao.
Katika majibu yake Zitto alisema: “Kwanza nataka
niwahakikishie watu wa Kigoma msiwe wanyonge… mna uwezo wa kutoa rais wa nchi
hii.
“Nimefanya kazi kubwa
katika ubunge, nimeleta mabadiliko mengi kuanzia bungeni mpaka jimboni. Nadhani
inatosha na hata nikiongezewa miaka mingine sitaweza kufanya yale yaliyonishinda
katika kipindi cha miaka 10.
“Kama Mungu ataniweka mpaka mwaka 2015, sitagombea
ubunge tena kwa sababu kazi niliyofanya inatosha.Natangaza rasmi kuwa nitagombea
urais kupitia chama changu cha Chadema, bila kusababisha msuguano wowote na
sitaki kuingia katika historia ya kurudisha nyuma harakati za upinzani kushika
dola.
“Nataka kuleta changamoto
mpya, nitawaeleza watu wa chama changu nia hiyo na nitatoa hoja za msingi. Hata
kama sitapata ridhaa yao, lakini huo ndiyo msimamo wangu. Iwapo chama kikiona
sistahili au sifai, nitakubaliana na uamuzi huo. Watu wengi wanadhani urais ni
cheo, hawajui kuwa ni nafasi ambayo inakufanya ufanye vitu ambavyo ni vikubwa na
vya maendeleo kwa wananchi.
”
Alipoulizwa kuwa mwaka
2015 atakuwa na miaka 39, hivyo kukosa sifa ya kugombea urais kwa mujibu wa
Katiba alijibu: “Nadhani nina uwezo wa kuwa rais, sidhani kama Katiba inaweza
kumzuia mtu mwenye uwezo asigombee na ndiyo maana ninaamini kuwa kipengele cha
kuwa na miaka 40 kitabadilishwa katika Katiba Mpya.”
Mwananchi
No comments:
Post a Comment