Saturday 6 October 2012

TAMKO LA JOHN MNYIKA KUHUSU WIKI YA VIJANA

TAARIFA KWA UMMA
Tarehe 4 Oktoba 2012 Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fennela Mukangara amezungumza na vyombo vya habari kueleza kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Taifa ya Vijana. Waziri ameeleza kuwa maadhimisho hayo yatahusisha maonyesho yatakayoanza tarehe 8 na kufikia kilele chake tarehe 14 Oktoba 2012 kwenye kilele cha mbio za Mwenge na kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere mkoani Shinyanga. Waziri ameeleza kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maonyesho na maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete. WAZIRI AELEZE HATUA ILIYOFIKIWA KATIKA KUANZISHA BARAZA LA VIJANA, BENKI YA VIJANA NA KUPANUA WIGO WA AJIRA KWA VIJANA Nikiwa mmoja wa vijana wa Tanzania na mbunge kijana sikubaliani na utaratibu mzima ulivyopangwa wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt Fennela Mukangara kutoa ratiba ya maonyesho na maadhimisho mengine bila kueleza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwa vijana katika maadhimisho kama hayo mwaka 2011 na pia kuweka mkazo katika maonyesho katika Mkoa mmoja badala ya masuala na matukio muhimu yenye kugusa maisha ya vijana wa katika maeneo mbalimbali nchini mijini na vijijini. Hivyo, natoa mwito kwa vijana katika maeneo mbalimbali nchini kutokubaliana na utaratibu huo wa kuweka kipaumbele katika maonyesho zaidi badala yake wafanye maadhimisho kwa kuweka kipaumbele masuala na matukio yenye kugusa maisha ya vijana na mustakabali wa taifa. Vijana tuitumie wiki hiyo kutafakari masuala ya msingi baina yetu ili tuweze kutimiza wajibu lakini wakati huo huo tuzifuatilie mamlaka zingine zinazohusika na masuala ya vijana kwa upande wao ikiwemo serikali katika ngazi zote kuhusu utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa kwa vijana kwa nyakati mbalimbali katika mwaka 2011. Kwa upande wangu, naitaka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ieleze hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa ahadi kipaumbele kuhusu ajira kwa vijana na uundwaji wa Baraza la Taifa la Vijana kama ilivyoniahidi bungeni mwaka 2011 na nyingine kuzirejea bungeni mwaka 2012. Kuhusu masuala ya ajira, tulipendekeza bungeni na Wizara ikakubaliana nasi kuanzisha Benki ya Taifa ya Vijana ili kuwezesha vijana wasioweza kumudu masharti ya kibenki katika mfumo wa kawaida wa kibenki kuweza kupata mitaji kwa masharti nafuu kwa ajili ya kujiajiri. Aidha, tulipendekeza na Wizara ikakubali kushirikiana na Wizara zingine ili kuwe na mfumo wa kuwezesha wahitimu wa vyuo kutumia vyeti vyao kama dhamana kuweza kukopa katika mabenki kwa ajili ya kujiajiri. Kuhusu uundwaji wa Baraza la Taifa la Maendeleo ya Vijana, serikali iliahidi kwamba mchakato wa kuundwa kwa baraza hilo ungekamilika katika mwaka wa fedha 2011/2012, hata hivyo mpaka kipindi hicho kinamalizika mwezi Juni 2012 na kuanza kwa mwaka mwingine wa fedha 2012/2013 ahadi hiyo haijatekelezwa. Baraza la Taifa la Maendeleo ya Vijana likianzishwa litaweza kuwaunganisha vijana bila kujali tofauti zao zingine katika kushughulikia vipaumbele 1 mbalimbali vya vijana ikiwemo katika masuala ya elimu, ajira, afya, michezo na maisha ya vijana kwa ujumla. MAADHIMISHO YA WIKI YA TAIFA YA VIJANA YASIFUNIKWE NA KILELE CHA MBIO ZA MWENGE Oktoba 8 mpaka 14 kila mwaka vijana bila kujali itikadi wanapaswa kuungana kote nchini kuadhimisha wiki ya taifa ya vijana. Hata hivyo, toka wiki hii ilipoanzishwa na Serikali mwaka 2003 imekuwa ikiadhimishwa bila mwitikio wa kiasi cha kutosha katika ngazi mbalimbali isipokuwa katika maeneo ambayo wiki hii imekuwa ikiadhimishwa kitaifa kwa kufanya maonyesho ya namna mbalimbali. Hivyo, nia ya taarifa hii ni kuhimiza vijana, serikali na wadau mbalimbali ili maadhimisho ya mwaka huu yawe na hamasa na maana zaidi kwa maisha ya vijana wa Tanzania na Taifa kwa ujumla. Aidha, maadhimisho ya kila mwaka ya wiki ya vijana yamekuwa yakichanganywa pamoja na kilele cha mbio za Mwenge na Maadhimisho ya siku ya Mwalimu Nyerere kitaifa. Matokeo yake wiki ya vijana imekuwa ikifunikwa na shamrashamra za mbio za Mwenge na hatimaye kupoteza malengo ya msingi ya kushughulikia masuala yanayowagusa vijana moja kwa moja. Pia zaidi ya maadhimisho ambayo yatafanyika kitaifa Shinyanga ni vyema mkazo ukawekwa katika kufanya maadhimisho katika ngazi mbalimbali hususani wilayani. Hivyo maafisa maendeleo wa vijana wa wilaya walau mwaka huu wajitokeze kutembelea vikundi vya vijana,kuratibu matukio ya asasi za vijana na kuhamasisha mijadala ya vijana kuhusu mustakabali wao na taifa kwa ujumla. Taarifa hii inalenga pia kutoa mwito kwa vijana nchini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya wiki ya taifa ya vijana ya mwaka huu itakayoanza Oktoba 8 ambayo kilele chake kitafikia Oktoba 14. Kila kijana wa Tanzania afanye walau kitu kimoja katika wiki hii kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya jamii-kama ni kusaidia wasiojiweza, kufanya usafi wa mazingira, kufanya majadiliano kuhusu mustakabali wa vijana na taifa, kuonana na viongozi kuzungumza nao kuhusu maendeleo katika maeneo yao kuhusu masuala ya elimu, ajira, afya, ukuzaji wa vipaji vya vijana, michezo, ushiriki wa vijana katika uongozi na mengineyo. Wiki hii ni muhimu kwa sababu kwa upande mmoja, vijana ndio kundi linaloathirika zaidi na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayojiri nchini kwetu na duniani kwa ujumla. Kwa upande mwingine vijana ndio chachu ya mabadiliko katika taifa lolote duniani kutokana na nguvu, ubunifu, na uwingi wetu
.
Imetolewa tarehe 5 Oktoba 2012 na:
John Mnyika MB

No comments:

Post a Comment

Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU