Thursday, 4 October 2012

MIAKA michache iliyopita niliandika makala ndefu sana nikiwashauri Watanzania wenzangu waliokuwa wanapigania sana vyama viungane ili kuwa na upinzani dhidi ya chama tawala na hatimaye kukiangusha chama tawala.
Naomba nikupitishe kwa kifupi sana msomaji wa kona hii kwenye makala ile ya Oktoba 8, 2008.

Niliamua kutumia makala nzima kueleza kwa kinagaubaga mawazo yangu kuhusu ushirikiano wa vyama vya upinzani ambao ulikuwa ukipigiwa upatu sana na Watanzania kwa muda mrefu. Siku hiyo niliwaambia kwamba ni vema ushirikiano wa vyama vinne vya upinzani (CHADEMA, CUF, NCCR-MAGEUZI na TLP) ukavunjika kwa masilahi ya taifa.


Nilieleza jinsi vyama vya upinzani vilivyoungana Kenya lakini baada ya kuing’oa KANU kulizuka mgogoro wa chama hiki kudai kupewa mawaziri wachache, kile kikidai kunyimwa wizara nyeti, hiki hapa kikidai makubaliano yamekiukwa na mambo kadha wa kadha mpaka wakagombana. Walisambaratika na kumlazimisha Rais aliyetokana na upinzani kuanzisha ushirikiano mpya na Rais aliyeondoka madarakani na hivyo kufifisha vita dhidi ya ufisadi na kusababisha serikali iliyokuwa madarakani ionekane ya ufisadi sawa na ile serikali iliyokuwa imepita.


Huo ndiyo ushirikiano wa vyama vya upinzani unaotafutwa na Watanzania?


Niliwatahadharisha Watanzania kwamba hatuhitaji ushirikiano wa vyama vya upinzani wenye lengo la kuing’oa CCM madarakani. Tunahitaji Tanzania mpya yenye kutoa fursa kwa kila raia kufaidi rasilimali za nchi hii na kujiletea maendeleo bila kujali katokea kundi gani.


Ushirikiano wa CHADEMA, CUF, NCCR na TLP hautafanikisha hayo.


Niliwashauri Watanzania tuwaruhusu wapinzani wavunje ushirikiano wao halafu wajijenge kama chama kimoja kimoja na ndipo tutakapoona chama chenye mwelekeo wa kuleta maendeleo tukipe kura.


Siku hiyo nilisema: “Natamani chama kama CHADEMA, ambacho kimejipambanua hivi karibuni kuwa chama makini chenye sera nzuri zilizopata kusifiwa hata na Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake na ambacho hivi karibuni kimewaonyesha Watanzania kwamba kumbe inawezekana kuiondoa CCM na tukaongozwa na chama kingine na kujipatia maendeleo ambayo hatukuwahi kuyaota wakati wote wa CCM, kipate kukubalika toka kwa Watanzania.


Wakipokee na kukipa nafasi ya kujipanua na mwaka 2010 kuwe na uchaguzi wenye ushindani kama tuliokuwa tunaushuhudia Tarime.


Vyama vingine viendelee kusimamisha wagombea urais, ubunge na udiwani kwa kuwa ni haki yao lakini mchuano uwe kati ya vyama viwili kama tulivyoona kule Tarime na hapo ndipo tutakuwa tunaelekea huko kwenye maendeleo.


Hayo yalikuwa baadhi tu ya maneno niliyoyasema wakati huo. Ni kama CHADEMA waliisoma makala ile kwa makini na kuielewa kwa kuwa muda mfupi baadaye walitangaza kuvunja ndoa ya upinzani na kuanza kujiimarisha kama chama peke yake chenye malengo ya kuchukua dola kwa kutumia sera zake chenyewe na kuepuka mtego wa kuungana na baadaye kuanza kupigana ni sera za chama gani kwenye ushirikiano zitekelezwe.


Wakaanzisha kile kilichojulikana kama Operesheni Sangara ambayo kwa kiwango kikubwa ilikidhoofisha sana chama tawala sanjali na vyama vingine vya upinzani.


Watanzania wakaanza kuielewa CHADEMA kama chama. Februari 11, 2009 nikaandika makala nyingine yenye kichwa cha habari, “CHADEMA na CUF wanahitaji msaada wako.”


Katika makala ile nikaomba kura ya maoni ikiwa vyama hivyo viwili viungane ama viendelee kujijenga kila kimoja kivyake! Wengi wakasema kila chama kijijenge kivyake, sababu zilikuwa nyingi na zote niliziandika katika makala iliyofuata.


Operesheni Sangara ilikuwa kama mashambulizi ya anga vitani. Mashambulizi ambayo siyo siri kwamba yamevidhoofisha mno vyama vikubwa kama CCM na CUF.


Ushahidi wa hili ni matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambapo CHADEMA ilipaa kutoka majimbo mtano ya ubunge iliyoyapata 2005 mpaka 23 mwaka 2010.


Wabunge viti maalumu kutoka 6 mpaka 25. Halmashauri za wilaya zinazoongozwa na CHADEMA kutoka vitatu mpaka saba.

Kura za urais kutoka laki sita mpaka mpaka milioni 2 na ushee, madiwani idadi ikaongezeka zaidi ya mara tano.
Kuimarika huku kwa CHADEMA hakuwezi kutokea bila kuviathiri baadhi ya vyama.


CCM kwa mfano majimbo yote ya CHADEMA yaliyoongezeka yalitoka mikononi mwa CCM, halmashauri zote zilizoongezeka kuongozwa na CHADEMA zilitoka mikononi mwa CCM, kura za urais zilipoongezeka zilipungua za CCM na CUF, kambi rasmi ya upinzani bungeni sasa ikapokwa mikononi mwa CUF ambayo imeiongoza kambi hiyo tokea mwaka 1995 na uongozi wa kambi sasa ukachukuliwa na CHADEMA.


Ruzuku ya CCM sanjali na ya CUF zinapungua wakati ya CHADEMA ikiongezeka kutoka milioni 60 kwa mwezi hadi milioni 230 kwa mwezi. Watanzania wakazidi kuipenda CHADEMA na wito wangu katika makala ile wa kuwataka Watanzania wakikumbatie hiki chama kama chao na kukiimarisha tayari kwa kukifanya chama mbadala wa kilichoko madarakani ukaonyesha kupokelewa na kutekelezwa barabara.

Safari ya CHADEMA kuelekea Ikulu ikaanza rasmi.


Ulipotokea uchaguzi mdogo Arumeru Magharibi, CHADEMA iliingia kwenye uchaguzi huo na kumbukumbu ya kipigo (hata kama kilikuwa cha haramu kama ilivyothibitishwa na mahakama hivi karibuni). Nikiwa mmoja wa viongozi wa chama tena nikiwa ndiye mwenyekiti wa mkoa wa Arusha ambamo ndimo kulikuwa na uchaguzi huo mdogo wa Arumeru, ilibidi kukaa na kufanya maamuzi.


Jambo la kwanza tulinuia hakuna kushindwa Arumeru kwa kuwa mtanange ilikuwa umekuja nyumbani ingelikuwa ni aibu kushindwa tena hata kama ushindi wa CCM ungelikuwa wa magumashi kama ambavyo imefanya siku zote.


Tukamuacha katibu mkuu wa chama akiwa na makamanda wengine katika kuhakikisha kampeni zinaanza na mikakati mingine ya kawaida ya kampeni zetu inaendelea.


Uongozi wa mkoa ukaungana na Mwenyekiti Taifa, Mkurugenzi wa Raslimali Taifa na Mkurugenzi wa Fedha Taifa, tukakaa pamoja kuandaa mkakati wa pekee wa ushindi ikiwa ni pamoja na kupata fedha na raslimali zingine kwa ajili kuendesha kampeni.


Ni katika kukaa wakati huo ndipo tulipokuja na wazo la M4C ama “Movement for Change” ama “Vuguvugu la Mabadiliko” kwa lugha yetu adhimu ya Kiswahili. M4C ikanuia kukikabidhi chama kwa wananchi. Wazo lilelile nililolizungumza kwenye makala yangu mwaka 2008.


Wanachama wakaipokea M4C nchi nzima. Wakachanga pesa na rasilimali nyingine na kiukweli kilichonishangaza zaidi ni kitendo cha wana CCM wengi wa chini kuipokea M4C na kuipa sapoti kubwa.


Katika uchaguzi wa Arumeru Mashariki wana CCM walifanya kazi ya ziada kuibeba CHADEMA. Walitupatia kura zao na za ndugu zao lakini zaidi walifichua hujuma nyingi sana zilizokuwa zinaandaliwa na CCM juu yetu. Tukapata ushindi wa kishindo!

Tukaikabidhi M4C kwa chama taifa na likawa sasa ni vuguvugu la nchi nzima. Kamati Kuu ikaamua kwa makusudi kuiboresha M4C ili itembee kwa mpangilio nchi nzima. Wakaamua kwamba sasa M4C ya kitaifa izinduliwe Dar es Salaam ili kufuta propaganda ya kwamba CHADEMA ni chama cha kaskazini tu.
Kutoka kwenye uzinduzi Dar es Salaam kwa makusudi kamati kuu ilikuwa imeelekeza M4C ielekee Mtwara na Lindi, eneo la ukanda wa Pwani ya kusini ambako CCM imekuwa ikidanganya watu kwamba CHADEMA haiwezi kwenda kwa sababu ni eneo la Waislam wengi na CHADEMA ni chama cha Wakristo.


Kazi iliyofanywa huko na M4C ya CHADEMA wanaoweza kusimulia vizuri ni kina Bernard Membe, George Mkuchika, Mathias Chikawe, Hawa Ghasia na wenzao ambao walikimbia majimboni kwenda kushuhudia. Kule CHADEMA ilifuta utawala wa CUF na CCM uliodumu miaka mingi.


Ili usipate shida ya kuniamini mimi au wale wasioitakiwa mema CHADEMA, ni vizuri ukaenda mwenyewe kufuatilia na kujua CHADEMA inaendeleaje huko kwa sasa.


M4C inafanyaje kazi. Imegawanywa katika vikosi vinne na awamu nne tofauti.


Kwanza hutangulia kikosi cha tathmini kinachokwenda kukagua hali ya chama na uongozi wa wake.


Hiki huweza kuja na majibu yanayoonyesha chama kiko katika hali gani na ni maeneo gani yanahitaji kuongezewa uzito.


Baada ya ripoti yao huja kikosi cha hamasa ambacho hufanya mashambulizi ya anga kwa njia ya mikutano ya hadhara kwa ajili ya kuhamasisha na kuingiza wanachama wapya.


Baadaye huja kikosi cha tatu ambacho kazi yake ni kusimamia uchaguzi tangu ngazi ya matawi mpaka kata.


Na mwisho huja kikosi cha mwisho ambacho hutoa mafunzo kwa viongozi waliochaguliwa kuwafanya wakijue chama waijue katiba ya chama, kanuni za uendeshaji chama, taratibu na maadili ya viongozi na wanachama ili waweze kuongoza vizuri chama kwa mujibu wa katiba, kanuni na maadili chama. Na vikosi hivyo vinapoondoka, vinaacha viongozi wa matawi na kata wakishuka kuweka kusimika viongozi wa misingi na mabalozi wa nyumba kumi wa CHADEMA. Wapi CCM itaponea? Wapi CUF itatokea? Hapo ndipo CCM ilipokiona kifo chake na CUF ikaanza kunusa kuzidi kudumaa kwake.


Unapomsikia leo Mwenyekiti wa CCM taifa anajiwahi wahi kusema CCM haifi kabla hajaulizwa, ni kile kile alichokisema Ansbert Ngurumo Jumapili iliyopita kwamba ni kama mlevi ambaye amelewa chakali na anatembea barabarani kwa kuyumba yumba na kuanguka hovyo, anapopishana na watu anaona wakimshangaa anaanza kupaza sauti: “Nani kasema mimi nimelewa? Sijalewa mimi!”


Kikwete kasoma nyuso za Watanzania na alipofika ukumbini akasoma nyuso za wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama chake, kama mlevi akaona wajumbe wakishangaa jinsi alivyochoka na chama kinamfia mikononi mwake. Kama yule mlevi akaanza kupaza sauti: “Kina nani wanasema CCM inakufa? CCM haifi bali wanaoiombea kifo watakufa wao na kuiacha imara!”


Naam, kupitia M4C CCM inakiona kifo chake kinavyokuja kwa hakika tena chafanya haraka. CUF nao wanaziona dalili za kunyauka kwani watabaki na mzizi mmoja tu ule wa Pemba ambao kwa kibaiolojia hauwezi kupitisha maji na madini ya chumvichumvi ya kuulisha mti mkubwa wa nchi nzima uitwao Chama cha Wananchi (CUF).


Ndiyo maana M4C ilipohamia Morogoro, Iringa, Dodoma, Singida na Manyara, ilibidi CCM na serikali yake watumie nguvu za dola kuizima na kuifanya isiendelee ili wenyewe wabaki madarakani.


Lakini niliwahi kusema huko nyuma baadhi ya watu wakanishambulia. Kwamba CHADEMA kina mkono wa Mungu maana hata yeye amechoka kuona watanzania wakiteseka hivi, ameleta mkombozi. Mbinu ya kutumia dola imeshindwa baada ya kifo cha Mwangosi. Sasa wamebuni kitu kipya. CCM wanaungana na CUF kuikabili M4C ya CHADEMA.


Ni bahati mbaya kwamba katika mkakati wao wameamua kuanzia Arusha. Walidhani kwa kuwa Arusha ni ngome ya CHADEMA na vijana wa Arusha hawana mchezo linapokuja suala la kutetea chama chao, wakadhani watawachokoza halafu CHADEMA watajibu kwa kuwafanyia vurugu na kisha serikali ya CCM iseme, “Mikutano ya kisiasa kwa sasa imekuwa chanzo cha uvunjivu wa amani.


“Kwa hiyo serikali imesitisha mikutano ya vyama vyote mpaka hapo hali itakapotulia.”


Itatulia lini, anajua waziri wa mambo ya ndani na jeshi lake la polisi na usalama wa taifa. Kwa kufanya hivyo watakuwa wamezuia M4C isiendelee. Ndugu yangu Mtatiro, wewe ni rafiki yangu sana. Nimeandika makala kadhaa kukutetea ulipokuwa unashughulikiwa pale Mlimani kwa sababu za kisiasa. Lakini katika hili sitakubaliana nawe niko tayari uniseme utakavyosema.


Ili kuonyesha kwamba ni mkakati, Mtatiro ulikuwa Dar es Salaam wakati ‘advance team’ yenu ilipokuja Arusha kuhamasisha ujio wa Ibrahim Lipumba, mheshimiwa mwenyekiti wenu taifa. Walifanya mikutano michache, mimi nilishuhudia mmoja tu pale Mbauda Sokoni ambapo walihutubia mkutano uliohudhuriwa na wananchi 11. Walikuwa wakihutubia kwa amani tele. Shida ilikuja pale walipokuta wamachinga wakiwa katika harakati za kujitwalia kwa nguvu kiwanja cha wazi kilichouzwa kifisadi kwa mtu binafsi.


Uuzaji ambao ulisababisha meya wa Arusha wakati huo ajiuzulu. Walikuwa wameziba barabara iendayo Kilombero sokoni. Gari la matangazo la CUF likaja.


Wakawaomba wageuze na kutumia barabara nyingine. Hawakutaka wakawa wanalazimisha kupita pale wakiimba nyimbo za CUF na kuwaonyesha ishara za chama chao.


Wamachinga wachache wakaamua kuwaonyesha alama ya CHADEMA pengine kuwaonyesha kwamba sisi wengine ni wanachama wa CHADEMA kwa hiyo hatuna haja ya kuonyeshwa alama za CUF.


Mtu mmoja aliyekuwa kwenye gari la matangazo la CUF akaamua kuwaonyesha wamachinga wale alama ya vidole vya kuonyesha matusi. Hapo ndipo wamachinga walipokasirika na kuwarushia mawe. Kumbe ni mtego uliopangwa, saa hiyo hiyo Mtatiro akarusha kwenye mitandao kwamba Wanachadema wamewashambulia wana CUF.


Baadaye wameleta Coaster zaidi ya nane kuja kuhudhuria mkutano wao wa Lipumba. Wakiwa njiani huko walipoulizwa na watu ambao hawakujua kama ni CHADEMA wakawa wanasema wanakwenda Arusha kulipiza kisasi cha watu wao kupigwa na CHADEMA. Wamekuja, Lipumba kahutubia hao watu wake aliowatoa Dar es Salaam na wana Arusha wasiozidi 100.


Kahutubia kwa amani kaondoka na hakuna badiliko lolote! Magazeti ya kesho yake hayakupata hata kuiweka habari yao ukurasa wa mbele isipokuwa yale ya wabia wao CCM ambayo yalidiriki kusema eti diwani wa CHADEMA ahamia CUF wakati wakijua huyo mtu alifukuzwa uanachama na CHADEMA na kupoteza hata udiwani. Anakuwaje diwani wa CHADEMA? Kwa hiyo V4C ilijifia kabla hata haijaanza kama walivyotabiri waandishi wenzangu.


Na mkakati wa pamoja kati ya CCM na CUF nao umefeli kabla ya majaribio jijini Arusha. Labda niwashauri wakaanzie huo mkakati Pemba
 

No comments:

Post a Comment

Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU