Tuesday, 2 October 2012

Mbunge awachochea wananchi Karatu

 
MBUNGE wa Karatu, Mchungaji Israeli Natse (CHADEMA), amewahamasisha wananchi wake wa Kata ya Baaray, Tarafa ya Eyasi kuwacharaza viboko watendaji wa vijiji na kata kutokana na tuhuma za kuchukua rushwa na kuruhusu wafanyabiashara wa vitunguu kukata miti na kulima katika chanzo cha maji cha Qangded.
Mchungaji Natse alitoa kauli hiyo juzi wakati akihutubia wananchi katika Kijiji cha Jobaj ambacho ni miongoni mwa vijiji saba vinavyotegemea chanzo hicho cha maji.
Alisema uamuzi wa kuwacharaza viboko watendaji hao, unatokana na ulegelege unaoonyeshwa na Serikali ya Rais Jakaya Kikwete katika kusimamia sheria na kanuni za utumishi.
Mchungaji Natse yupo jimboni akiambatana na wabunge wengine na viongozi kadhaa wa CHADEMA kutembelea vijiji mbalimbali kuangalia sakata la uharibifu wa mazingira lililofanywa na wafanyabiashara katika bonde la Mto Eyasi.
Wabunge wengine alioambatana nao ni Kabwe Zitto (Kigoma Kaskazini), Rose Kamili (Viti Maalum), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Pauline Gekul (Viti Maalum) na Joshua Nasari (Arumeru).
Akiwahutubia wananchi katika vijiji saba vinavyozunguka bonde hilo la Eyasi, Natse alisema uharibifu huo unachangiwa kwa kiasi kikubwa na udhaifu wa Serikali ya Rais Kikwete.
Natse alieleza kuwa uharibifu uliofanywa na wafanyabiashara watano katika vyanzo hivyo vya maji katika bonde la Ziwa Eyasi, ulianza kushughulikiwa vizuri na Mkuu wa Wilaya hiyo, Daudi Ntibenda kwa kuwakamata waharibifu hao, lakini maagizo ya kichama yaliyotolewa na kuongezwa shinikizo la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, yalifanya watuhumiwa hao kuachiwa bila masharti.
Alisema hali hiyo inatokana na ulegelege wa Serikali ya Rais Kikwete ambapo watumishi wake wa ngazi za kati na chini wanajiamulia mambo bila kujali madhara ya uamuzi huo wanaoufanya kwa wananchi na hata kwa chama chao cha siasa wanachokitumikia.
“Naomba Kikwete anisikie na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo. Ulegelege wa serikali hii ndio unaotaka kuhatarisha maisha ya wakazi wanaozunguka bonde hili kwa kuwalinda wafanyabiashara wa vitunguu waliofyeka miti katika vyanzo vya maji na wao kuweka mashine 32 za kuvutia maji kwenda kwenye mashamba yao kwa kuwa wanaifadhili CCM,” alisema Natse.
Alifafanua kuwa wanatoa muda wafanyabiashara hao waondoke wenyewe kabla harakati hazijaanza kwa kutumia wananchi kuwatoa hapo kwa kuwa hakutakua na woga wa mabomu ya machozi wala virungu vya polisi wakati wa kuwaondoa.
Watuhumiwa wanaotajwa kuhusika na kuharibu chanzo hicho kikuu cha maji ni katika Kata ya Mang’ola ambao walikamatwa na mkuu wa wilaya na kuwekwa rumande kabla ya kuagizwa kuwaachia huru ni Waziri Saidi, Christopher Msemo, Loema Gilong, Girigisi Gidobad, Mamoya Muhindi na Sudi Omary.
Naye Kamili akihutubia wakazi wa Kijiji cha Jobag, aliwahamasisha kutozubaa kwa kuwa wao ndio wataathirika wa uharibifu huo, hivyo akawataka akina mama na vijana kufunga vibwebwe na kuhamia katika vyanzo hivyo kuondoa mashine hizo na kulilinda eneo hilo kwa muda wote.
Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU