Friday 5 October 2012

Sumaye ateta na Chadema


NI KUHUSU MUSTAKABALI WAKE KISIASA

SIKU chache baada ya kushindwa katika uchaguzi wa ndani kwenye nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amekutana na viongozi wa Chadema ikidaiwa kuwa ni kujadili pamoja na mengine, uwezekano wa kuhamia huko ili agombee urais katika Uchaguzi Mkuu ujao 2015.

 
Sumaye ambaye anatajwa kuwa alikuwa na mpango wa kuwania urais kupitia CCM, alishindwa katika uchaguzi wa kuwania ujumbe wa Nec, baada ya kupata kura 481 dhidi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), Dk Mary Nagu aliyepata kura 648.
 
Taarifa zilizothibitishwa na baadhi ya viongozi wa Chadema, zimeeleza kuwa Sumaye hakuridhishwa na mchakato wa uchaguzi huo wa Nec na kwa matokeo hayo, alikutana na viongozi wa Chadema kujadili mustakabali wake kisiasa.
 
Jana, mjumbe mmoja wa Kamati Kuu ya Chadema, ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini, alithibitisha Sumaye kukutana na viongozi wa Chadema. Hata hivyo alisema hawajafikia mwafaka.
 
Alisema mawasiliano ya Chadema na Sumaye yalianza mara tu baada ya matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Septemba 30, mwaka huu yaliyomwengua kigogo huyo kwenye kinyang’anyiro hicho.
 
“Ni kweli kuna watu wa CCM tumewasiliana nao baada ya uchaguzi ule (wa Nec) na Sumaye tunawasiliana naye pia lakini siwezi kusema tumefikia wapi,” alisema mjumbe huyo na kuendelea: “Suala kwamba amekubaliwa kujiunga na Chadema au la, nadhani huu ni uamuzi wake. Ninachoweza kusema ni kwamba vikao vilikuwepo na vinaendelea kukaliwa.”
Alisema baada ya matokeo ya Hanang’ na hali ya kisiasa ndani ya CCM, Chadema kimekuwa kikiwasiliana na Sumaye na kikubwa ambacho kinajionyesha ni kada huyo wa CCM kutoridhishwa na hali ya mambo ndani ya chama chake.
 
Mjumbe huyo wa Chadema alisema chama hicho Wilaya ya Hanang’ kinaandaa mkutano maalumu wa kuwapokea wanachama wapya wa CCM, wengi wao wakiwa baadhi ya walioanguka kwenye uchaguzi wa Nec wilayani humo.

Habari zaidi zimeeleza kuwa Chadema kimepanga siku yoyote juma lijalo, kuwapokea wanachama wapya kutoka CCM, baadhi wakiwa wale walioshindwa kwenye uchaguzi wa ndani ya chama hicho uliofanyika wilayani Hanang’.

Mmoja wa watu wa karibu na Sumaye alisema anachojua ni kwamba Chadema wanamtaka Sumaye na siyo Sumaye kukitaka chama hicho cha upinzani.

“Wamekuwa wakimfuatafuata mara nyingi na mazungumzo ya aina hiyo si mageni baina ya Sumaye na Chadema. Ila ninachoweza kusema, safari hii chochote kinaweza kutokea kutokana na hasira alizonazo (Sumaye). Ngoja tusubiri, atafanya mkutano na waandishi Jumapili.”

Sumaye, Mbowe wazungumza
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Sumaye alisisitiza kuwa atazungumzia masuala yote yanayohusiana na uchaguzi huo wa Hanang’ atakapokutana na waandishi wa habari, Dar es Salaam.

 
“Nitakutana na waandishi wa habari kuzungumzia kilichotokea naomba tu mwendelee kunipa muda,” alisema Sumaye na kuongeza kuwa alikuwa akijiandaa kwa safari ya kwenda Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema asingependa kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yeye si msemaji wa Sumaye... “Sitaki kumzungumzia Sumaye. Mimi si msemaji wake. Tumsubiri yeye azungumze kuhusu hilo.”
Kada wa CCM Hanang’ anena

Katika hatua nyingine, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Hanang’, Goma Gwaltu amekionya chama hicho kuwa kisipodhibiti vitendo vya rushwa katika chaguzi zake, kitakufa.
Gwaltu alisema jana kwamba kwa mazingira yaliyopo sasa ndani ya CCM bila hatua kali kuchukuliwa, kiongozi asiye na fedha hawezi kushika uongozi na ndiyo sababu anaungana na wana-CCM wengine katika wilaya hiyo, ambao wanafikiria kukihama chama hicho.
 
“Kama wewe una nia ya kuendelea na siasa siyo rahisi kushinda hapa Hanang’ ukiwa hukubaliani na watu fulani, sasa mimi naona ni bora tu kutafuta chama kingine kwani siyo dhambi,” alisema Gwaltu bila kuwataja ambao wanataka kuhama CCM.
 
Hata hivyo, Gwaltu alisema kwa upande wake, hafikirii kuendelea na mambo ya siasa wala kulalamika makao makuu ya CCM kuhusiana na alichokiita hujuma alizofanyiwa

Kwa habari kamili tembelea:
 

No comments:

Post a Comment

Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU