Tuesday 18 September 2012

PINDA AZOMEWA MWANZA, MKUTANO WAKE WANUSURIWA NA MBUNGE WENJE WA CHADEMA

VIJANA MWANZA WAIMBA ‘PEOPLE’S POWER, HATUITAKI CCM’

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya kushindwa kuhutubia maelfu ya wakazi wa Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza kwa muda kutokana na wananchi wengi kumzomea.

Kiongozi huyo alikumbana na kisanga hicho cha aina yake akiwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina pamoja na Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Evarist Welle Ndikilo.

Pinda na viongozi hao, walikumbana na zomeazomea hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Sahara jijini hapa, ikiwa ni hitimisho la ziara ya Waziri Mkuu huyo ya siku saba mkoani Mwanza.

Chanzo cha Pinda na viongozi hao kuzomewa mkutanoni hapo, ilitokana na kile kilichoonekana kuwepo kwa kero nyingi zilizodaiwa kushindwa kupatiwa ufumbuzi na Serikali ya CCM chini ya Rais Jakaya Kikwete.

Kitendo hicho cha wananchi kilimlazimisha Pinda kushindwa kuhutubia kwa muda, huku akionekana kujawa jazba.

Sababu nyingine ya wananchi kuzomea, ni hatua ya Pinda kuwaambia wananchi hao watoke mjini waende vijijini wakalime waachane na mambo ya upinzani wa kisiasa.

Pinda alitoa kauli hiyo baada ya kundi la vijana mkutanoni hapo kuonesha alama ya V, bendera ya CHADEMA na nyimbo za Peoples, Power.

Kwa mazingira hayo, askari wa polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), waliokuwa na silaha nzito za kivita aina ya SMG, mabomu na marungu waliokuwepo mkutanoni hapo, walianza kuwatishia kuwapiga wananchi hao kwa lengo la kumlinda kiongozi huyo.

Baada ya kuzidi zomeazomea hiyo, Waziri Mkuu, Pinda alilazimika kumuita mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (CHADEMA), aliyekuwa meza kuu, kisha kusema: "Nyamazeni basi!. Wenje...hii ndiyo serikali ya siku chache zijazo. Kwa namna hii naona hamuwezi, maana itakuwa ni vurugu asubuhi hadi jioni". Akazomewa kisha wakaimba hatutaki CCM, hatutaki CCM. .

Baada ya kuona hivyo, Pinda akacheka na kusema: "Hahahaaaaa, hata mkiimba peoples power, CCM ndiyo inayowaongoza". Akazomewa tena kisha Pinda akashindwa kuendelea kuzungumza jukwaani.

Akahutubia mkutanoni hapo, Pinda aliwataka wananchi hao waache ushabiki wa kisiasa, na kwamba halmashauri ya jiji la Mwanza inayoongozwa na CHADEMA, ndiyo itapaswa kulaumiwa kama itashindwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi wake.

"Hapa jiji la Mwanza linaongozwa na CHADEMA. Meya wa CHADEMA, mwenyekiti wa Mipango miji wa CHADEMA, Naibu Meya ni wa CHADEMA. Lakini kama wameshindwa kuweka mipango mikakati ya kuwasaidia tutasema hawafai," alisema kisha akazomewa kwa mara nyingine.

Baada ya zomeazomea hiyo kuonekana kumwelemea Waziri Mkuu huyo, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Ndikilo alilazimika kuingilia kati kwa kusema: "Wanaozomea tunawafahamu, na tunawafahamu waliowaleta hapa ili mje kufanya nini". Akazomewa.

Hata hivyo, baada ya hali kutulia kidogo, Pinda aliendelea kuhutubia huku akiwataka wananchi wa jiji la Mwanza waondoke mjini waende vijijini wakalime, jambo lililoonekana pia kuwakasirisha wananchi wengi kisha kumzomea tena.

Ingawa Pinda alilazimika kutumia muda mfupi kutoa hotuba yake, aliwaomba wana Mwanza washirikiane kuleta maendeleo yao, na kwamba iwapo tatizo ni Mkurugenzi wa jiji suala hilo litaangaliwa.

Aliwaomba wadumishe amani iliyopo hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Serikali kupambana na vitendo vya uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, ili kuweza kuzua samaki wadogo wasivuliwe kisha kuharibu mazalia ya rasilimali hiyo.

"Jambo jingine ninalotaka kuwaeleza hapa leo ni hili la uvuvi haramu. Samaki ndani ya Ziwa Victoria wameisha...na hii ni kwa sababu ya uvuvi usiozingatia sheria. Tushirikianeni kupambana na vitendo hivi", alisema Pinda kisha akazomewa tepa.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU