Thursday 20 September 2012

CHOPA NNE KUONGEZA NGUVU KATIKA AWAMU NYINGINE YA M4C

Ni awamu nyingine ya M4C
Zitashambulia mikoa minne
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinakusudia kuendelea na Operesheni Sangara kwa nguvu kubwa ikiwemo kutumia helkopta nne na kuongeza idadi ya magari katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuyafikia maeneo mengi ambayo miundombinu yake ni mibovu.

Chama hicho kitatumia helikopta hizo wiki mbili zijazo kitakapoendelea na operesheni hiyo yenye kauli mbiu ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) katika Mkoa wa Iringa.

Operesheni hiyo ilitarajiwa kuanza mkoani Iringa Agosti 28, mwaka huu, lakini ilisitishwa baada ya chama hicho kukubaliana na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, kwamba iendelee baada ya kumalizika kwa sensa ya watu na makazi.

Baada ya sensa kumalizika, Chadema kilitangaza kuisitisha operesheni hiyo kufuatia tukio la mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, mkoani Iringa, Daudi Mwangosi kwa bomu wakati polisi wakikabiliana na wa wafuasi wa chama hicho kwenye ufunguzi wa tawi katika kijiji cha Nyololo katika wilaya ya mufindi, mkoani Iringa.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Morogoro jana baada ya kumalizika kwa kikao cha Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Mwenyekiti wake, John Heche, alisema kuwa operesheni hiyo inatarajia kuanza tena ndani ya wiki mbili zijazo na itanzia mkoani Iringa na kuendelea katika mikoa mingine.

“Kwa taarifa yenu, sasa tutaruka angani na chopa nne kuongeza nguvu Operesheni Sangara, tutaendelea na Mkoa wa Iringa ambako tuliisimamisha kutokana na mauaji ya Mwangosi,” alisema Heche na kuongeza: “Tukitoka hapo tunapiga mikoa mingine.”

Heche alisema lengo la kutumia helikopta hizo nne ni kuwafikia wananchi wengi kuanzia ngazi ya kitongoji ili kuwaeleza mambo mbalimbali, yakiwemo maovu yanayofanyika nchini.

Mwenyekiti huyo wa Bavicha alisema hatua hiyo inatokana na baadhi ya sehemu katika wilaya mbalimbali na mikoa nchini kutofikika kwa njia ya gari kutokana na ubovu wa mindombinu ya barabara ambayo katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru Serikali ya CCM imeshindwa kuiboresha.

Akizungumzia maazimio ya kikao cha kamati ya Utendaji cha Bavicha, alisema kuwa mstakabali wa vijana wa taifa hili hivi sasa unakabiliwa na na changamoto nyingi kutokana na serikali ya CCM kushindwa kusimamia mambo mbalimbali.

Alisema kutokana na hali hiyo, Kamati Tendaji ya Bavicha imeiagiza sekretarieti yake kuunda kikosi kazi au kamati ya kufanya utafiti zaidi ili kujua kwa kina matatizo ya vijana hususani kuanzia masuala ya kuporomoka kwa elimu, ukosefu wa ajira na kutoa ushauri juu ya mstakabali wa taifa baada ya mwaka 2015.

Heche alisema kuwa Bavicha itaendelea kuwaunga mkono walalahoi nchini, wakiwamo wamachinga na matatizo yanayowakabili wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu katika kupata mikopo yao pamoja na kuvifuatilia viwanda ambavyo vilikuwa vikitoa ajira mbalimbali na hivi sasa vimegeuka kuwa mabanda ya mifugo.

Mbali na maazimio hayo, pia baraza hilo limetoa tahadhari kwa vyombo vya dola na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, kuepusha kauli za vitisho zinazohatarisha amani ya nchi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha Zanzibar, Sharifa Suleiman, alisema vurugu zote zinazotokea kwenye majukwaa ya kisiasa kwa sehemu kubwa zinatokana na propaganda zinazofanywa na CCM kwa lengo la kuichafua Chadema na kupendekeza kuwa ni muhimu CCM kikaondolewa kwenye orodha ya vyama vya siasa nchini.

“Tumeshuhudia wananchi wakiendelea kunyanyaswa na vyombo vyao vya dola wanavyovilipa kwa kodi zao,” alisema Sharifa.

Akifafanua zaidi alisema vyombo vya dola viondokane na mfumo wa kinyanyasaji wa kujichunguza vyenyewe na kulitaka Jeshi la Polisi kujisafisha kabla wanachi hawajaamka na kukataa kukandamizaji unaofanywa na baadhi ya askari wake bila kuchukuliwa hatua zozote.

Chadema ilianzia Operesheni Sangara katika Mkoa wa Morogoro na ilitarajia kuendelea nayo katika mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Njombe.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU