TAMKO LA CHAMA KUKANUSHA SHUTUMA ZA CHAMA
CHA CUF KUFANYIWA VURUGU NA CHADEMA.
Ndugu
wananchi na wanahabari,
Siku ya terehe 27 Alhamisi Septemba 2012 chama cha wananchi CUF walitoa taarifa ya malalamiko kwa vyombo vya habari na mitandao kuwa wanachama wa CHADEMA wamewafanyia vurugu kwa kuwapiga mawe na kuwa jambo hilo limehamasishwa na viongozi wa chama katika mkoa wa Arusha pamoja na Mhe Godbless Lema.
Wote
tunafahamu kuwa siku hiyo hiyo katika viwanja vya soko la Kilombero
wafanyabiashara ndogo ndogo walikuwa wamevamia na walikuwa wakijigawia maeneo,
baada ya eneo la awali walilopewa la viwanja vya NMC kushindwa kuwachukua
wafanyabiashara wote na halmashauri kushindwa kutoa majibu kwa wafanyabiashara
hawa ambao waliwaambia wote waende NMC.
Kwanza
tunapenda kutoa pole kwa viongozi wa CUF kwa jambo hili lililowapata. Wao kama
watu na Watanzania wenzetu tunawapa pole sana.
Pili, CHADEMA
inakanusha kuhusika na jambo hili. Hii si tabia ya CHADEMA na kamwe haiwezi kuwa
tabia ya CHADEMA kufanya siasa chafu za namna hiyo. CHADEMA tunajali sana amani
na upendo, na hii ndiyo tabia na makuzi yetu
Watanzania.
Katika
mazingira haya, CHADEMA tunachukua fursa hii kuvikaribisha vyama vyote mathalani
CUF, Arusha ni yetu sote na tutumie demokrasia vizuri kufanya kazi nzuri ya
siasa kwa ajili ya kusababisha na kuleta matumaini kwa Watanzania hawa ambao
serikali ya chama cha mapinduzi imeshindwa
kuwaletea.
CHADEMA
hatuna shida na ushindani wa kisiasa katika mazingira ya kidemokrasia kwa maana
ndio wakati pia wa wananchi kupima na kujua nani mkweli na ama nani anafanya kwa
dhati ya kweli. Hivyo tunawakaribisha CUF karibuni Arusha na wala wasitafute
kisingizio cha kuegemea ili CUF ianze kutajwa tajwa kwa kutumia mgongo
wetu.
Sambamba na
hili, CHADEMA mkoa wa Arusha tumesikitishwa sana na tamko la CUF lilitolewa na
Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na haki za BInadamu Mhe Abdul Kambaya, tamko
lenye matisho na lugha isiyofaa. Moja na maneno ya tamko hilo wamesema, nukuu
“Uwezo wa kuwafanya tutakavyo tunao na kwa sababu wameanza tunaweza
kumaliza”. Wakazi wa Arusha na Watanzania wapime na waone, haya si
maneno yanayoweza kutoka kwenye kichwa cha mtu anayefikiri vizuri, mtu
anayeipenda nchi yake na kuheshimu utawala wa sheria. Zaidi ya hapo tamko hilo
limesema pia, “Ile ngangari kwa polisi tunaweza kuwahamishia wao wakose pa
kukaa”.
Katika yote
haya, niwaombe wakazi wa Arusha, Wanachadema na hata wanachama wa vyama vingine
tuwapende na tuwakaribishe CUF Arusha na sote tufanye kazi ya siasa kwa nguvu za
hoja. CUF wanaweza kufanya hicho wanachotaka kufanya lakini CHADEMA kamwe hatupo
tayari kwa vurugu ya aina yoyote, aidha tunawakaribisha kwa moyo mmoja na kama
wapo tayari basi tufanye siasa zenye tija na manufaa kwa wakazi wa
Arusha.
Aidha nitoe
onyo kali sana kwa mamluki ambao wamekuwa wakijifanya kondoo kumbe ndani ni mbwa
mwitu. Mara kadhaa watu hawa wamekuwa wakisababisha fujo ili kukifanya CHADEMA
kionekane kuwa ni chama cha vurugu. MAMLUKI ni sumu, tukimgundua na
kumthibitisha mtu wa aina hiyo katikati yetu tutamtangaza mbele ya jamii kuwa
yeye ni sumu na kuomba wananchi wamtenge maana anapingana kwa kuleta hila na
unafiki kwenye kazi ya kuwakomboa Watanzania. Niwatangazie mamluki hamtatuweza
na tutawagundua tu.
Mwisho,
tunapoelekea kwenye marudio ya uchaguzi mdogo kwenye kata za Daraja II kwa
Arusha mjini na Bangata kwa wilaya ya Arumeru Magharibi, nirudie kusema maneno
ya Mhe Lema kuwa iwapo viongozi na watumishi wa umma watajihusisha na kushiriki
kwa kufanya kampeni za kisiasa wakiwa wanatumia magari na vifaa vingine vya
serikali watu hawa tutawakamata na tutawapeleka huko wanakostahili kupelekwa
wezi na vibaka wengine. Hii ni tahadhari tunamaanisha kweli na wananchi wote
wawe makini “wakamate mwizi” lengo likiwa ni kuweka adabu kwa
watumishi na viongozi umma wanaovunja sheria ya utumishi wao kwa umma na
matumizi ya rasilimali kwa namna isivyotakiwa kisheria. CHADEMA tutashiriki
chaguzi hizi na tunawaomba wakazi wote wa maeneo haya tushiriki kwa utulivu na
amani.
WANACHADEMA
wote tuendelee kuwa majasiri, tusiwe waoga na tusimamie kweli na haki.
“Hakuna
kulala Mpaka Kieleweke”
Amani Sam
Golugwa
KATIBU WA
CHADEMA MKOA WA ARUSHA: golugwa@gmail.com
No comments:
Post a Comment