Serikali imetakiwa
kumdhibiti na kumuondoa, kisha kuibomoa nyumba ya Mbunge wa Viti Maalum (CCM),
Mchungaji Getrude Lwakatare.
Rai hiyo imetolewa na
Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.
Taarifa kwa vyombo vya
habari jana ilieleza kuwa, wakati raia wengine wakibomolewa nyumba ambazo kama
ilivyo ya Mchungaji Lwakatare, zilijengwa kinyume cha sheria, Mbunge huyo
amehamia na kuishi kwenye nyumba yake.
Julai mwaka huu, nyumba za
wananchi waliojenga katika maeneo tengefu ya ufukwe wa Jangwani, mto Ndumbwi na
mto Mbezi, zilibomolewa katika operesheni iliyoendeshwa na Baraza la Mazingira
la Taifa (Nemc).
Operesheni ambayo
ilihusisha takriban nyumba 15 na kuta nane. Lakini nyumba ya Mchungaji Lwakatare
haikuguswa.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa, aliwahi kuwaambia
waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa, nyumba hiyo haikubomolewa kutokana na
pingamizi la mahakama.
Nyumba inayotajwa kuwa mali
ya Mchungaji Lwakatare, imejengwa kwenye viwanja namba 2019-2020 Kawe Beach,
katika fukwe za bahari ya Hindi.
Viwanja hivyo vinadaiwa
kupatikana kwa ushirikiano wa Mchungaji Lwakatare na Frank Mushi.
Mdee alisema wakati kigogo
huyo (Lwakatare) amehamia kwenye nyumba yake kwa matangazo na mbwembwe, mto
Ndumbwi, bahari na mazingira kwa ujumla yameharibiwa, lakini zaidi kuwepo raia
waliobomolewa kwa mujibu wa sheria hizo.
Mdee alinukuu Sheria ya
Mazingira, sura 191 ya mwaka 2004, fungu 57(1), inasema hairuhusiwi kufanya
shughuli zozote za kudumu za kibinadamu ndani ya mita 60.
Mita hizi ni ambazo kwa
asili yake zinaweza kuhatarisha au kuathiri ulinzi na utunzaji wa mazingira,
utunzaji wa bahari, kingo za mto, bwawa au mwambao wa asili wa
ziwa.
Sheria nyingine ni ya
ardhi, namba 4 ya mwaka 1999, sura 113, fungu la 7 (1) (d), ikieleza kwamba eneo
lolote lililo ndani ya mita 60 kutoka kingo ya mto na bahari, linatakiwa
kutangazwa kama ardhi hatari au kuhifadhiwa.
Na pale inapotokea kuwa
masharti ya sheria moja yanapingana na masharti ya Sheria ya Mazingira, kuhusu
mambo yanayohusu usimamizi wa mazingira, sheria hiyo inatumika, kwa mujibu wa
fungu 232 la sheria ya mazingira sura 191 ya mwaka 2004.
”Kutokana na hali hii,
serikali inatakiwa kujinasua katika mwendelezo wa tafsiri wanayoipata wananchi
kuwa imetekwa na kuwekwa mfukoni na watu wachache wenye uwezo,”
alisema.
Aliongeza,” maana wanaona
kuwa huu ni mwendelezo wa serikali kuwa na kigugumizi pale sheria zinapovunjwa
na vigogo serikalini, au watu wenye fedha wanaoshirikiana na baadhi ya viongozi
wa serikali na chama tawala kufanya ufisadi.”
Alisema hali ilivyo sahihi
inadhihirika kuwepo kundi la wanaojiona wapo juu ya sheria, huku wanyonge
wakishughulikiwa.
”Ni wakati kwa mawaziri
wanaohusika na masuala ya ardhi na mazingira kuwaeleza Watanzania kulikoni
wananchi wa hali ya chini kuvunjiwa nyumba wakati Mchungaji Lwakatare, ambaye
uharibifu wake ni wa hatari kuliko waliovunjiwa akitamba mtaani, ”
alidai.
Mdee alitafsiri kitendo
hicho kama ni Mchungaji Lwakatare kutamba kuwa yuko juu ya sheria na hakuna
mamlaka yoyote yenye uwezo wa kumzuia kufanya alichofanya.
”Ni aibu kwa Taifa kuwa na
viongozi wa aina hii! Viongozi ambao wako tayari kutumia fedha, hila, mamlaka na
dhamana za uongozi walizopewa, kuhalalisha haramu, ni janga kwa mstakabali wa
taifa letu,” alisema.
Waziri wa Ardhi , Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa, hawakupatikana kuelezea juu ya tamko la
Mdee.
Mawaziri hao walikaririwa
kwa nyakati tofauti wakisema nyumba zote zilizojengwa kando kando ya fukwe za
bahari na mito zitabomolewa
No comments:
Post a Comment