VIJANA
MWANZA WAIMBA ‘PEOPLE’S POWER, HATUITAKI CCM’
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda,
jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya kushindwa kuhutubia maelfu ya wakazi
wa Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza kwa muda kutokana na wananchi wengi
kumzomea.
Kiongozi huyo alikumbana na
kisanga hicho cha aina yake akiwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Clement
Mabina pamoja na Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Evarist Welle Ndikilo.
Pinda na viongozi hao,
walikumbana na zomeazomea hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya
Sahara jijini hapa, ikiwa ni hitimisho la ziara ya Waziri Mkuu huyo ya siku saba
mkoani Mwanza.
Chanzo cha Pinda na
viongozi hao kuzomewa mkutanoni hapo, ilitokana na kile kilichoonekana kuwepo
kwa kero nyingi zilizodaiwa kushindwa kupatiwa ufumbuzi na Serikali ya CCM chini
ya Rais Jakaya Kikwete.
Kitendo hicho cha wananchi
kilimlazimisha Pinda kushindwa kuhutubia kwa muda, huku akionekana kujawa
jazba.
Sababu nyingine ya wananchi
kuzomea, ni hatua ya Pinda kuwaambia wananchi hao watoke mjini waende vijijini
wakalime waachane na mambo ya upinzani wa kisiasa.
Pinda alitoa kauli hiyo
baada ya kundi la vijana mkutanoni hapo kuonesha alama ya V, bendera ya CHADEMA
na nyimbo za Peoples, Power.
Kwa mazingira hayo, askari
wa polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), waliokuwa na silaha nzito za
kivita aina ya SMG, mabomu na marungu waliokuwepo mkutanoni hapo, walianza
kuwatishia kuwapiga wananchi hao kwa lengo la kumlinda kiongozi
huyo.
Baada ya kuzidi zomeazomea
hiyo, Waziri Mkuu, Pinda alilazimika kumuita mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje
(CHADEMA), aliyekuwa meza kuu, kisha kusema: "Nyamazeni basi!. Wenje...hii ndiyo
serikali ya siku chache zijazo. Kwa namna hii naona hamuwezi, maana itakuwa ni
vurugu asubuhi hadi jioni". Akazomewa kisha wakaimba hatutaki CCM, hatutaki CCM.
.
Baada ya kuona hivyo, Pinda
akacheka na kusema: "Hahahaaaaa, hata mkiimba peoples power, CCM ndiyo
inayowaongoza". Akazomewa tena kisha Pinda akashindwa kuendelea kuzungumza
jukwaani.
Akahutubia mkutanoni hapo,
Pinda aliwataka wananchi hao waache ushabiki wa kisiasa, na kwamba halmashauri
ya jiji la Mwanza inayoongozwa na CHADEMA, ndiyo itapaswa kulaumiwa kama
itashindwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi wake.
"Hapa jiji la Mwanza
linaongozwa na CHADEMA. Meya wa CHADEMA, mwenyekiti wa Mipango miji wa CHADEMA,
Naibu Meya ni wa CHADEMA. Lakini kama wameshindwa kuweka mipango mikakati ya
kuwasaidia tutasema hawafai," alisema kisha akazomewa kwa mara
nyingine.
Baada ya zomeazomea hiyo
kuonekana kumwelemea Waziri Mkuu huyo, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Ndikilo
alilazimika kuingilia kati kwa kusema: "Wanaozomea tunawafahamu, na tunawafahamu
waliowaleta hapa ili mje kufanya nini". Akazomewa.
Hata hivyo, baada ya hali
kutulia kidogo, Pinda aliendelea kuhutubia huku akiwataka wananchi wa jiji la
Mwanza waondoke mjini waende vijijini wakalime, jambo lililoonekana pia
kuwakasirisha wananchi wengi kisha kumzomea tena.
Ingawa Pinda alilazimika
kutumia muda mfupi kutoa hotuba yake, aliwaomba wana Mwanza washirikiane kuleta
maendeleo yao, na kwamba iwapo tatizo ni Mkurugenzi wa jiji suala hilo
litaangaliwa.
Aliwaomba wadumishe amani
iliyopo hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Serikali kupambana na
vitendo vya uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, ili kuweza kuzua samaki wadogo
wasivuliwe kisha kuharibu mazalia ya rasilimali hiyo.
"Jambo jingine ninalotaka
kuwaeleza hapa leo ni hili la uvuvi haramu. Samaki ndani ya Ziwa Victoria
wameisha...na hii ni kwa sababu ya uvuvi usiozingatia sheria. Tushirikianeni
kupambana na vitendo hivi", alisema Pinda kisha akazomewa tepa.
Tanzania
Daima
No comments:
Post a Comment