TENDWA AIBUKA, ATISHIA
KUWAFUTIA USAJILI
CHAMA cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), kimeipinga tume ya kuchunguza mauaji ya aliyekuwa mwandishi
wa Channel Ten, Daudi Mwangosi, iliyoundwa na Waziri wa Mambo wa Ndani, Dk.
Emmanuel Nchimbi, kwa maelezo kuwa inaongozwa na jaji asiye na
sifa.
Kimesema kuwa Jaji huyo
mstaafu, Stephen Ihema, anafahamika ni mtu asiyejua kazi, kwani ameshindwa kutoa
hukumu katika kesi zaidi ya 300.
Akizungumza na waandishi
jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria, Katiba na Haki za
Binadamu wa chama hicho, Tundu Lissu, alisema kutokana na Jaji Ihema kutoweza
kazi, hata Jaji Bernard Luanda alipata kumkosoa kwa kutoa waraka kwa majaji wote
mwaka 2005.
“Kama mnafuatilia taarifa
za hivi karibuni, Ihema ni mmoja wa majaji waliopo kinyume cha sheria na Katiba.
Aliteuliwa kuwa jaji enzi za Benjamin Mkapa, ilipofika mwaka 2003 kwa sababu
hakuwa anajua sheria,” alisema.
Lissu ambaye ni Mbunge wa
Singida Mashariki, aliongeza kuwa Ihema hajui kazi ya ujaji na kwamba
alisharundika zaidi ya kesi 300 ambazo anashindwa kuziandikia hukumu. Na kuwa
mtu ambaye anajulikana kutokuwa na uwezo wowote wa kufanya kazi ya
kisheria.
“Ndugu zangu na hili naomba
nirudie maana wasiseme tumeanza maneno yetu, mwaka 2003 kabla mimi sijawa mbunge
kuna mtu anaitwa Joram Alute, ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Singida kwa sababu
ya ubovu wa Jaji Ihema, Joram alimwandikia Rais Mkapa barua ya kumuomba
kumuondoa Jaji Ihema Mahakama Kuu, kwa sababu hakuwa na uwezo wowote wa kufanya
kazi ya ujaji.
Miaka karibu 10 wana CCM,
Joram Alute, si CHADEMA, alisema hawezi kazi, aidha ni mvivu au hajui namna ya
kuandika hukumu, hafai kuwa jaji,” alisema Lissu.
Aliongeza kuwa mwaka 2005
Jaji Ihema alikuwa amemaliza mkataba wa kwanza na kupewa mwingine wa kazi ya
ujaji, hali ambayo ilimfanya Jaji Bernard Luanda (sasa Jaji wa Mahakama ya
Rufaa), baada ya kuandikiwa na Jaji Manento kuwa Ihema amepewa mkataba wa ujaji,
aliandika waraka uliosambazwa kwa majaji wote kuwa Ihema si jaji kwa mujibu wa
Katiba.
Alisema kwa mujibu wa
sheria za nchi, majaji wanateuliwa, hivyo Jaji Ihema kupewa mkataba ni kinyume
cha sheria na katiba.
Lissu alieleza kuwa hata
alipopelekwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, tume hiyo ilikuwa ni ya
kuficha uchafu na madhambi ya viongozi, kwani ilikuwa kimya kwa miaka yote huku
viongozi wakishiriki kufilisi taifa.
Alisema kutokana na maelezo
hayo ni dhahiri kuwa Ihema hana uwezo na pia maadili yake ni ya mashaka, kwani
hilo linafahamika ndani ya mahakama.
Pamoja na hilo, alisema
tume hiyo imeundwa kwa lengo la kurekebisha mambo baada ya Jeshi la Polisi
kukamatwa mchana kweupe wakifanya mauaji.
“Ni tume ambayo lengo lake
si kuchunguza mauaji, ni kuondoa hii picha ya mauaji yaliyofanywa na Jeshi la
Polisi hadhaharani…hii ndivyo tunavyoiangalia.
Kwa kuwa si tume ya
kuchunguza mauaji sisi kama chama hatutaiunga mkono na tutawashauri wananchi wa
Tanzania, wawe wanachama wetu, wasiwe wanachama wetu, wasiiunge mkono,”
alisema.
Nchimbi
akosolewa
Lissu alisema kwa mujibu wa
sheria ya kuunda tume za uchunguzi mwaka 1962 sura ya 29, anayepaswa kuunda tume
ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutoa hadidu rejea na kwamba
kulingana na utaratibu huo si jukumu la waziri kuunda tume.
Alisema tume za aina hiyo
zinatoa ripoti kwa rais au zinaweza kutoa taarifa hadharani endapo rais
ataelekeza hivyo katika hadidu rejea.
“Hivyo kwa matukio makubwa
ya kitaifa yanayotokea, kisheria ni jukumu la rais, si jukumu la waziri ambaye
anawasimamia watuhumiwa wa hicho kinachotakiwa kuchunguzwa.
Kwa hiyo katika upeo huo wa
kisheria, Waziri Nchimbi hana mamlaka ya kuunda tume ya kuchunguza mauaji hayo,”
alisema.
Lissu alifafanua kuwa
walioua ni polisi ambao inawezekana waliamriwa waue na wakubwa zao kisiasa
(waziri) au kiutendaji (IGP na maofisa wengine wa jeshi), hivyo kama unachunguza
mauaji yaliyofanyika waziwazi, inawezekana yamefanywa kwa amri za kisiasa au
kiutendaji.
Hivyo alihoji kama tume
hiyo ina uwezo wa kumhoji waziri au IGP na kusema kuwa: “Tume hii ni danganya
toto, ya kitchen party, pengine na ya marafiki, ili kuondoa picha mbaya kwa
Jeshi la Polisi,” alisema.
Wajumbe wake
waguswa
Lissu alisema Naibu
Kamishna wa Polisi, Isaya Mungulu, kutoka makao makuu hana uwezo kwa kumuita
waziri au IGP kwa ajili ya kumhoji kuhusiana na mauaji hayo.
Kuhusu mtaalamu wa mabomu,
Wema Wapo, kutoka Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) alihoji kuwa
anakwenda kuchunguza kitu gani kisichojulikana, kwani katika picha muuaji
anajulikana.
“Inaonekana ni bomu la
machozi ambalo alipigwa nalo, ambalo limemchanachana. Sasa ni kitu gani
kisichojulikana. Sasa unaita mtaalamu achunguze mlipuko upi ambao haujulikani?”
alihoji.
Kwa upande wa Theopili
Makunga kutoka Jukwaa la Wahariri (TEF) na Pili Mtambalike kutoka Baraza la
Habari Tanzania (MCT), alisema hao ni waandishi wa habari na kuhoji iwapo wana
utaalamu wa kuchunguza vifo.
“Hii ni tume ya marafiki,
yenye lengo la kukosha mauaji yaliyofanywa na marafiki, kwa vyovyote vile hii si
tume halali ya kuchunguza mauaji ya Mwangosi,” alisema Lissu.
Hadidu rejea
zapingwa
Lissu alihoji ni mtu gani
asiyefahamu chanzo cha mauaji hayo, kwani vyombo vya habari vimemuonyesha
kupitia picha, hivyo kuhoji tume hiyo inakwenda kuchunguza kitu
gani.
Kuhusu swali kama kweli
kuna uhasama kati ya polisi mkoani Iringa na waandishi, alihoji iwapo tume hiyo
inakwenda kuchunguza mauaji ama uhasama.
Kwa upande wa swali kama
nguvu iliyotumika na polisi ilikuwa sahihi, alisema kuwa hilo ni suala la
kisheria na pia kunahitajika ushahidi.
“Kuhusu swali linalohoji
mahusiano kati ya polisi na vyama vya siasa. Hili liko wazi kabisa kwa sababu
sijawahi kusikia Jeshi la Polisi limevunja mikutano ya CCM, kwa hiyo hapa
wanakwenda kuichunguza CHADEMA,” alisema.
Aliongeza kuwa iwapo
wanataka kuchunguza suala hilo kwa nini Mungulu yupo kwenye tume hiyo na hakuna
mtu wa CHADEMA wala Msajili wa Vyama vya Siasa au mwakilishi wake.
“Hii si tume ya kuchunguza
mauaji, ni ya kufunika mauaji haya…hatuwezi kukubaliana na tume hii,”
alisema.
Mbali na hilo, alisema kuna
haja ya kuchunguza matukio mbalimbali ya mauaji yaliyotokea hivi karibuni
likiwemo la Morogoro, Arusha, Igunga na Arumeru Mashariki.
“Matukio yote haya
hayajachunguzwa inavyostahili. Hatutaki mambo yaishe hivi hivi,”
alisema.
Mapendekezo
yao
Kutokana na hali hiyo,
alisema chama hicho kinamtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda tume ya uchunguzi wa
mauaji ambayo itaongozwa na majaji waadilifu na kwamba itakuwa bora iwapo
watatoka Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu, ambao watafanya uchunguzi wa
wazi.
“Katika tume hiyo mashahidi
watakuwa wakiitwa hadharani. Tume za aina hii hazipo, lakini kwa mujibu wa
sheria Rais anaweza kuunda tume hiyo. Hatutaki uchunguzi wa kificho ambao
unaonesha polisi hawakukosea,” alisema.
Alieleza kuwa tume hiyo
itakuwa na mamlaka ya kumuita mtu yeyote isipokuwa rais. Na kwamba kwa kuwa
muuaji anajulikana, chama hicho kinataka askari wote waliohusika wakamatwe na
kufunguliwa kesi ya mauaji.
“Tunajua si wote walioua,
ila katika sheria kuna kitu kinaitwa common intension, mmoja ameua, lakini
alioshirikiana nao wanahusika. Hili linawezekana kwa kuwa kuna ushahidi,”
alisema.
Alisema iwapo rais hataunda
tume hiyo, kuna njia nyingi za kuendelea na suala hilo, na kusema hilo chama
kinapaswa kutoa kauli.
Wataka Nchimbi
ajiuzulu
Katika hatua nyingine,
Lissu alisema kutokana na tukio hilo, Waziri Nchimbi anapaswa kuwajibika kisiasa
kwa kujiuzulu, kwani hawezi kuendelea kuwa waziri na kuheshimika kutokana na
tukio hilo.
“Kama ana chembe ya
uadilifu afuate nyayo za Mwinyi (Ali Hassan Mwinyi) miaka 36 iliyopita ambaye
alijiuzulu uwaziri. Nchimbi hawezi kuwa waziri na kuendelea kuheshimika kama
anaongoza jeshi la wauaji. Akishindwa kujiuzulu rais amfukuze kazi,”
alisema.
Alieleza kuwa mauaji ya
aina hiyo ni ya kisiasa na kuongeza kuwa jeshi hilo limekuwa likifanya kazi kwa
niaba ya CCM.
Tendwa
aibuka
Mauaji ya Daudi Mwangosi,
anayedaiwa kuuawa kwa bomu na askari polisi mkoani Iringa, yamemuibua Msajili wa
Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, ambaye ametishia kuvifuta vyama
vinavyojihusisha na siasa za vurugu.
Katika mkutano wake na
waandishi wa habari jana, Tendwa ambaye alitumia muda mwingi kuwatisha CHADEMA
pia amelionya Jeshi la Polisi na kulitaka lifanye kazi zake kwa wajibu wa sheria
za nchi.
Tendwa ambaye ofisi yake
imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya upinzani kuwa inashindwa kutekeleza wajibu
wake kutokana na kuegemea upande wa Chama tawala cha CCM, alisema kuwa
demokrasia ya sasa imekua na kusababisha vifo vya raia wasio na
hatia.
Alisema hawezi kuvumilia
siasa za vurugu zinazohatarisha amani ya taifa lililopata uhuru wake miaka 50
iliyopita kwa kisingizio cha operesheni za ukombozi.
Tendwa alisema haoni haja
ya CHADEMA kuendelea na operesheni yao ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) wakati
huu ambao si kipindi cha uchaguzi, hivyo kutishia kukifuta chama hicho alichodai
mikutano yake imekuwa ikizusha vurugu.
Aliainisha kuwa kuanzia
mwaka jana hadi sasa mauaji kadhaa ya raia yametokea katika mikutano ya kisiasa
katika mikoa ya Arusha, Singida, Morogoro na Iringa na kwamba hali hiyo
haiwezekani kusema taifa ni huru.
Alisema kuwa Agosti 10
mwaka huu, mkutano wa vyama vya siasa na Jeshi la Polisi ulifanyika na
kuzungumzia masuala mbalimbali likiwamo la amani nchini, kufanyika kwa mikutano
ya vyama, wajibu wa vyama vya siasa kwa kufuata sheria za nchi na wajibu wa
Jeshi la Polisi nchini.
Tendwa aliongeza kuwa
kutokana na kuwapo kwa sheria ya mikutano ya vyama vya siasa nchini, ikitokea
chama chochote cha siasa kitaleta chuki na uvunjifu wa amani kitapaswa
kufutwa.
“Kutokana na hali
tuliyoifikia kwa sasa inatisha, hivyo vyama vya siasa viondoe uchochezi,”
aliongeza.
Pia amelitaka Jeshi la
Polisi kutimiza wajibu wake wa kulinda raia pamoja na mali zao na kuwataka
wavitumie vyombo vyao kwa ustaarabu.
DCI asuswa
Iringa
Jeshi la Polisi nchini
limeanza kuonja shuluba ya matukio yao kususiwa na waandishi wa habari, ambapo
jana Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, DCI Robert Manumba, alikuwa wa kwanza
kukumbwa na adha hiyo mkoani Iringa.
Waandishi wa habari
wameazimia kutoripoti taarifa zozote za jeshi hilo hadi hapo wale waliohusika
katika kusababisha kifo cha mwanahabari, Daudi Mwangosi, watakapokuwa
wamekamatwa na kuchukuliwa hatua.
Manumba ambaye jana alikuwa
akitaka kutoa taarifa za awali juu ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi, alijikuta
katika wakati mgumu baada ya wanahabari hao kugoma kabisa kwenda
kumsikiliza.
Pia waandishi hao wamekosoa
tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi,
wakisema haijakidhi haja wala kuzingatia uwiano, kwa kile walichoeleza kuwa
hakuna hata klabu moja ya waandishi wa habari iliyoshirikishwa.
Awali waandishi hao walitoa
masharti kwa DCI wakitaka awepo peke yake katika chumba cha mikutano lakini
Manumba alijitetea kuwa tamko alilotaka kutoa ni lazima na maofisa hao
walisikie.
“Jamani punguzeni jazba juu
ya hili, ninajua mna mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa hili na suala hili
limemgusa kila mmoja, hasa ninyi waandishi wa habari, hivyo naomba mnisikilize
na mjue tunataka kuwaambia nini,” alisema DCI Manumba bila
mafanikio.
Wakati huo huo, waandishi
wa habari mkoani hapa, walisema wakati tume iliyoundwa na Dk. Nchimbi haijaanza
kazi yake rasmi ni vema Kamanda wa Polisi mkoani humo akaachia madaraka yake kwa
muda ili kupisha uchunguzi huru.
Katibu wa Chama cha
Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, Frank Leonard, alisema mbali na kumtaka
Kamuhanda kujiuzulu pia ni wakati muafaka kwa tume iliyoundwa ikawahusisha na
viongozi wa klabu ya waandishi.
TUCTA yamlilia
Mwangosi
Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi Nchini (Tucta), limemlia aliyekuwa mwandishi wa kituo cha runinga
cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi, likisema alikuwa ni mchapa
kazi.
Katibu Mkuu wa Tucta,
Hezron Kaaya, alisema kuwa ni jambo la kusikitisha na kushangaza kwa mwandishi
kuuawa wakati akitekeleza majukumu yake.
“Kwa kweli Tucta kati ya
mambo ambayo yametuuma na kutusikitisha ni kifo cha Mwangosi kinachoripotiwa
kufanywa na Jeshi la Polisi, hasa kitendo cha kusambaratishwa mwili wake, kwani
hata mnyama anapouawa katika mawindo huwa hauawi kwa namna ile,”
alisema.
Kaaya aliongeza kuwa ni
jambo la kusikitisha kwa kuwa kifo kile kitachukua muda mrefu kwa Watanzania
kukisahau kwani hakuwa na kosa lolote alilolifanya mpaka kuuawa namna
ile.
Aliongeza kuwa kwa hali
ilivyo sasa taifa linaelekea pabaya, kwa sababu haki ya mnyonge haizingatiwi
tena na wenye nguvu, akitoa mfano kuwa wanyonge wanapodai haki yao jibu rahisi
ni kusambaratishwa kwa mabomu na virungu vya polisi.
Alisema endapo hali hiyo
itaachwa iendelee hivyo, kunaweza kutokea maafa makubwa kwa wananchi waliochoka
kuonewa na kudhulumiwa haki zao.
Kaaya alibainisha kuwa
Watanzania wengi wameuawa katika matukio ya kisiasa na hakuna hatua madhubuti
zilizochukuliwa kukomesha hali hiyo isiendelee kutokea, badala yake zinaundwa
tume ambazo hata hivyo hazijulikani zinakoishia zaidi ya kutumia fedha za walala
hoi.
Tanzania Daima
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment