BARAZA la Vijana la Chama
cha Demokrasia na Maendeleo, BAVICHA, limemtaka Rais Jakaya Kikwete na serikali
ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuiepusha nchi katika machafuko kwa kuwawajibisha
haraka viongozi wa dola katika Wizara ya Mambo ya Ndani kutokana na tuhuma za
unyanyasaji, mateso na mauaji kwa raia wasio na hatia endapo wao hawataki
kujitoa.
Waliotajwa wajiuzulu au
wawajibishwe na Rais kwa maslahi ya umma ni Waziri wa Mambo ya Ndani Dk. Emanuel
Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Saidi Mwema.
Aidha Mkuu wa Operesheni wa
Jeshi la Polisi Paul Chagonja, kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Faustin
Shilogile, Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, na wakuu wa
kikosi cha kutuliza ghasia mikoa hiyo wamependekeza washtakiwe.
Akisoma maazimio ya baraza
hilo la taifa lililofanyika mjini hapa kwa siku tatu, Mwenyekiti wa BAVICHA
Taifa, John Heche, alisema tayari serikali imeiweka nchi rehani kutokana na
kufumbia macho matukio hayo yanayoendelea kufanywa na vyombo vya
usalama.
“Mpaka sasa wananchi hawana
imani na serikali yao hususan Jeshi la Polisi na haya matukio yameubadilisha
ulimwengu jinsi polisi wanavyoendesha unyama kwa raia wasio na hatia kwa
visingizio visivyo na maana,” alisema Heche.
Akifafanua juu maazimio 10
yaliyofikiwa na ya baraza hilo, Heche alisema kwa muda mrefu Jeshi la Polisi
limekuwa likitumika kama kivuli cha Chama cha Mapinduzi kuficha uovu wake na
lenyewe kujificha kwa chama hicho.
“Uone nchi hii
inavyokwenda, huyu Kamuhanda aliua watu wanne Songea kumlinda kahamishiwa Iringa
nako amefanya hayo hayo mpaka sasa hajakamatwa, huyo Shilogile aliua hapa
Morogoro anafunikwafunikwa na hawa wote wamekuwa wakilindwa na makao makuu
kupitia mkuu wa operesheni jeshi la polisi Paul Chagonja ambaye anaeneza uongo
kwa umma kuwalinda polisi wenzie,” aliongeza.
Katika maazimio hayo
likiwemo la kuwataka kujiuzulu, kuwajibishwa au kufunguliwa kosa la mauaji kwa
mantiki ya ‘Common intention’ viongozi hao, BAVICHA pia lilimtaka Rais Kikwete
kuunda tume huru ya kiuchunguzi ya kimahakama katika makosa yote yaliyotokea
Arusha, Arumeru, Igunga, Ndago-Singida, Morogoro na Iringa.
Aidha baraza hilo
linakusudia kuunda kikosi kitakachotafiti matatizo ya vijana likiwemo suala la
elimu duni na ukosefu wa ajira na kutoa ushauri juu ya mustakabli wa taifa baada
ya 2015, kuendelea kuwaunga mkono walalahoi nchini wakiwemo machinga, na
imelaani CCM kuwatumia vijana katika mafunzo ya kijasusi kwani yanalenga
kulichafua taifa.
Mbali na maazimio hayo pia
baraza hili limetoa tahadhari kwa vyombo vya dola na Msajili wa Vyama vya Siasa
John Tendwa kuepusha kauli za vitisho zinazohatarisha amani ya nchi huku
wakimshauri kuifuta CCM kwa kufundisha ujasusi.
Kwa upande wake Makamu
Mwenyekiti wa BAVICHA Sharifa Suleiman alisema baraza limepitia na kuchambua kwa
kina mustakabali wa kisiasa, vijana na sintofahamu iliyopo na inayozidi
kudhihirika kuwa uongozi uliopo umeshindwa kuongoza hasa katika kusimamia
rasilimali za nchi kwa faida ya Watanzania.
Tanzania
Daima
No comments:
Post a Comment