MBUNGE wa Kigoma Kaskazini,
Kabwe Zitto na mwenzake wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), wamewaonya
viongozi na madiwani wa chama hicho wilayani Karatu kuwa hawatavumiliwa endapo
watashindwa kutatua tatizo la maji wilayani humo.
Vigogo hao walitoa msimamo
huo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wakiwahutubia wakazi wa mji wa Karatu
wakiwa wameongozana na Mbunge wa jimbo hilo, Mchungaji Israel Natse, katika
mkutano wa kuhamasisha maendeleo pamoja na ushiriki wa wananchi katika utoaji wa
maoni ya Katiba mpya.
Zitto ambaye pia ni Naibu
Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, alisema akiwa kama kiongozi wa chama pamoja na
Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Lissu, wametoa maagizo kwa viongozi
wao wa wilaya chini ya Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Lazaro Maasai, kwenda
kuzungumza na wananchi kwenye vijiji ambavyo mradi wa maji wa Kaviwasu
unapita.
Alifafanua kuwa lengo la
kwenda kuzungumza na wananchi hao ni kujua matatizo yaliyopo ambayo
yanasababisha mradi huo kutotoa huduma kwa kiwango kilichokusudiwa na kuyapatia
ufumbuzi mara moja ili watu waendelee kupata maji safi na ya
kutosha.
“Naomba niwambie wazi kama
hawatatekeleza maagizo haya tutawafukuza wote kwa kuwa hatutakubali kuona mradi
huo wa maji ulioasisiwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, wakati
akiwa mbunge wa jimbo hili unaharibiwa na watu wachache wenye tamaa ya fedha,’’
alisema.
Aliongeza kuwa wametembelea
maeneo hayo na kukutana na malalamiko mengi juu ya viongozi kushindwa kusimamia
vema majukumu yao na kuwataka wananchi wawaambie viongozi hao kuwa katika miradi
ya maendeleo hakuna siasa na ikibidi wawawajibishe kama watashindwa kutekeleza
majukumu yao.
Akizungumzia kuhusu
utoroshwaji wa fedha nje ya nchi unaofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali,
Zitto alisema tayari wana orodha ya Watanzania 27 ambao wanamiliki mamilioni ya
dola nje ya nchi ambayo waliyapata kwa njia zinazotia shaka.
Zitto alitaja kuwa miongoni
watuhumiwa hao yumo ofisa mmoja wa jeshi mstaafu ambaye hata hivyo hakumtaja
jina, akisema anamiliki akaunti nje ya nchi ikiwa na kiasi cha dola milioni
56.
Aliitaka serikali iwataje
wote wanaomiliki fedha nje na kuchukua hatua haraka, vinginevyo wao watawaweka
hadharani kwa umma ili nguvu ya wananchi ichukue mkondo.
Naye Lissu akizungumza
katika mkutano huo, aliwaonya wananchi wa Karatu wasikubali kuanza kurubuniwa
kwa kuchukua visenti vidogo vidogo na kuharibu historia yao nzuri ya mfano kwa
nchi hii.
Alisema vitendo vya
kuendekeza njaa katika masuala ya utendaji si desturi na mfumo wa chama hicho,
hivyo kuwatahadharisha wananchi kuwa kama kunatokea kiongozi ama mwanachama ana
matatizo hayo basi hakuna kufichaficha waelezane hadharani.
Kuhusu utoaji maoni kwenye
tume ya Katiba, Lissu aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kama
wanavyojitokeza kwenye mikutano ya chama hicho ili kutoa maoni yao.
“Naomba niwaambie wananchi
nyie mna historia kubwa toka nchi inapata uhuru mliishawahi kuchagua kiongozi
bila kupitia chama chochote, Chifu Sarwatt na mkambwaga mgombea wa TANU lakini
leo miaka 50 ya uhuru tunaambiwa bado hatujakomaa kuwa na wagombea binafsi, kwa
kutumia uandikwaji wa Katiba mpya jitokezeni mtoe maoni yenu,” alisema
Lisu.
Alifafanua kuwa
wasipojitokeza kutoa maoni kwa tume hiyo watakuwa wamechangia kuruhusu watu
wachache kuwaandikia Katiba ama vipengele vingi vya Katiba ya zamani
inayolalamikiwa vitabaki vilevile.
Tanzania
Daima
No comments:
Post a Comment