Wednesday, 3 October 2012

Kingunge nusura amng’oe Kikwete

MWENYEKITI wa Chama cha Mapunduzi, Rais Jakaya Kikwete, na sekretarieti yake wameponea tundu la sindano kung’oka baada ya mkongwe wa siasa nchini, Kingunge Ngombale Mwiru, kutangaza mgogoro wa katiba ya chama hicho ambao ungehatarisha nafasi yake.
Kingunge ambaye ameshika nafasi mbalimbali za uongozi nje na ndani ya chama, aliwasilisha hoja hiyo ya mgogoro wa katiba wiki iliyopita wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), iliyokuwa na ajenda ya kufanya uteuzi wa majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM.

Habari kutoka ndani ya NEC, zilizema kuwa mara baada ya Rais Kikwete kufungua mkutano huo, Kingunge alinyoosha mkono akitaka kuwasilisha taarifa.
Kabla ya kuruhusiwa, Rais Kikwete alimtaka mkongwe huo kuvuta subira ili atoe taarifa za vurugu za wakulima na wafugaji Loliondo na baada ya kumaliza kutoa taarifa hiyo kwa NEC, alimruhusu Kingunge kuzungumza.
Alipopata nafasi, Kingunge alianza: “Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani sana, nimesimama hapa kutangaza mgogoro wa Katiba.”
Aliendelea: “Tukijiridhisha kwamba katiba imevunjwa, lazima tujadiliane na tuchukue hatua kwa faida ya chama. Hivi sasa chama kiko kwenye harakati za uchaguzi ndani ya chama baada ya katiba ya chama chetu kufanyiwa marekebisho.
“Bahati mbaya sana marekebisho hayo yamefanywa na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu bila kupata baraka za Mkutano Mkuu kama katiba inavyotaka.
“Katiba yetu inasema marekebisho yoyote ya chama lazima yapate baraka za Mkutano Mkuu isipokuwa tu kama kuna dharula, lakini kwa bahati mbaya mabadiliko yaliyofanywa hayana baraka za Mkutano Mkuu na hili sio jambo la dharula.
“Kwa maana hiyo mchakato mzima wa uchaguzi unaoendelea ni batili, hivyo mchakato huo uvutwe na kuanza upya hadi hapo Mkutano Mkuu utakapopitisha marekebisho ya katiba,”
Alisisitiza: “Huo ni ukiukwaji mkubwa wa katiba uliofanywa na viongozi wa chama na ikithibika wamevunja katiba, wawajibishwe.”
Wakati Kingunge akitoa hoja hiyo ya kutaka mchakato mzima kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa ufutwe kwa madai ya kukiuka katiba, baadhi ya wajumbe walikuwa wakishangilia kumuunga mkono.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kuwa mara baada ya kuwasilisha hoja hiyo, wajumbe na meza kuu walizizima na baadaye Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, alisimama kujibu hoja hiyo.
Msekwa alianza kwa kusema kuwa yeye ndiye aliyeongoza kamati iliyosimamia marekebisho ya katika ya CCM ya mwaka 1977 na anajua vizuri kipengele alichotumia Kingunge kutangaza mgogoro wa katiba.
Msekwa alikisoma kifungu hicho ambacho kinasema: “Kusimamisha kwa maslahi ya CCM utumiaji wa kifungu chochote cha Katiba ya kuingizwa ndani ya Katiba, Uamuzi huo sharti uungwe mkono na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na Theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar. Hata hivyo Halmashauri Kuu ya CCM taifa, itafikisha uamuzi wake mbele ya Mkutano Mkuu wa CCM wa Taifa kwa uamuzi wa mwisho.”
Baada ya kusoma kifungo hicho, Msekwa alisema mabadiliko hayo ya katiba yalizingatia kifungu hicho na baadaye wajumbe wa pande mbili za muungano walipiga kura kuafiki mabadiliko hayo.
Kwa mujibu wa Msekwa, NEC sasa inawajibika kutoa taarifa mbele ya Mkutano Mkuu kuhusu mabadiliko hayo, hivyo hakuna katiba iliyovunjwa.
Ikumbukwe kuwa wakati wajumbe walipopiga kura kuridhia mabadiliko hayo, Kingunge alipiga kura ya hapana, kupinga mabadiliko hayo.
Duru za kisiasa ndani ya NEC, zilisema kuwa baadhi ya wajumbe walihoji sababu ya Kingunge kutaka kumng’oa Kikwete na serektari yake wakati ana uwezo wakati wowote kumwona mwenyekiti wa chama na kujadiliana naye kama kuna makosa.
“Bahati nzuri sana wajumbe wengine hawakusimama kuunga mkono, lakini jambo lenyewe lilikuwa baya, fikiria kama tungefuta mchato mzima na kuvunja sekretarieti maana yake CCM ingefia hapo,” alisema mmoja wa wajumbe wa NEC.
Baadhi ya madiliko yaliyofanywa katika katiba ya CCM ni pamoja na kuwaondoa wazee wastaafu (marais) katika vikao vya NEC na kuwapa nafasi ya kuunda baraza lao.
Mabadiliko hayo pia yameruhusu wana CCM kugombea NEC kupitia wilayani kwao ili kukisogeza chama mikononi mwa wananchi.
 
KUTOKA TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment

Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU