MBUNGE wa Karatu, Mchungaji
Israeli Natse (CHADEMA), amewahamasisha wananchi wake wa Kata ya Baaray, Tarafa
ya Eyasi kuwacharaza viboko watendaji wa vijiji na kata kutokana na tuhuma za
kuchukua rushwa na kuruhusu wafanyabiashara wa vitunguu kukata miti na kulima
katika chanzo cha maji cha Qangded.
Mchungaji Natse alitoa
kauli hiyo juzi wakati akihutubia wananchi katika Kijiji cha Jobaj ambacho ni
miongoni mwa vijiji saba vinavyotegemea chanzo hicho cha maji.
Alisema uamuzi wa
kuwacharaza viboko watendaji hao, unatokana na ulegelege unaoonyeshwa na
Serikali ya Rais Jakaya Kikwete katika kusimamia sheria na kanuni za
utumishi.
Mchungaji Natse yupo
jimboni akiambatana na wabunge wengine na viongozi kadhaa wa CHADEMA kutembelea
vijiji mbalimbali kuangalia sakata la uharibifu wa mazingira lililofanywa na
wafanyabiashara katika bonde la Mto Eyasi.
Wabunge wengine
alioambatana nao ni Kabwe Zitto (Kigoma Kaskazini), Rose Kamili (Viti Maalum),
Tundu Lissu (Singida Mashariki), Pauline Gekul (Viti Maalum) na Joshua Nasari
(Arumeru).
Akiwahutubia wananchi
katika vijiji saba vinavyozunguka bonde hilo la Eyasi, Natse alisema uharibifu
huo unachangiwa kwa kiasi kikubwa na udhaifu wa Serikali ya Rais
Kikwete.
Natse alieleza kuwa
uharibifu uliofanywa na wafanyabiashara watano katika vyanzo hivyo vya maji
katika bonde la Ziwa Eyasi, ulianza kushughulikiwa vizuri na Mkuu wa Wilaya
hiyo, Daudi Ntibenda kwa kuwakamata waharibifu hao, lakini maagizo ya kichama
yaliyotolewa na kuongezwa shinikizo la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, yalifanya
watuhumiwa hao kuachiwa bila masharti.
Alisema hali hiyo inatokana
na ulegelege wa Serikali ya Rais Kikwete ambapo watumishi wake wa ngazi za kati
na chini wanajiamulia mambo bila kujali madhara ya uamuzi huo wanaoufanya kwa
wananchi na hata kwa chama chao cha siasa wanachokitumikia.
“Naomba Kikwete anisikie na
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo. Ulegelege wa serikali hii ndio unaotaka
kuhatarisha maisha ya wakazi wanaozunguka bonde hili kwa kuwalinda
wafanyabiashara wa vitunguu waliofyeka miti katika vyanzo vya maji na wao kuweka
mashine 32 za kuvutia maji kwenda kwenye mashamba yao kwa kuwa wanaifadhili
CCM,” alisema Natse.
Alifafanua kuwa wanatoa
muda wafanyabiashara hao waondoke wenyewe kabla harakati hazijaanza kwa kutumia
wananchi kuwatoa hapo kwa kuwa hakutakua na woga wa mabomu ya machozi wala
virungu vya polisi wakati wa kuwaondoa.
Watuhumiwa wanaotajwa
kuhusika na kuharibu chanzo hicho kikuu cha maji ni katika Kata ya Mang’ola
ambao walikamatwa na mkuu wa wilaya na kuwekwa rumande kabla ya kuagizwa
kuwaachia huru ni Waziri Saidi, Christopher Msemo, Loema Gilong, Girigisi
Gidobad, Mamoya Muhindi na Sudi Omary.
Naye Kamili akihutubia
wakazi wa Kijiji cha Jobag, aliwahamasisha kutozubaa kwa kuwa wao ndio
wataathirika wa uharibifu huo, hivyo akawataka akina mama na vijana kufunga
vibwebwe na kuhamia katika vyanzo hivyo kuondoa mashine hizo na kulilinda eneo
hilo kwa muda wote.
Tanzania
Daima
No comments:
Post a Comment