Sumaye amtangazia vita Lowassa
• Mwenyewe asema wananchi wa Monduli ndiyo msuli wake
SIKU chache baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Fredereck Sumaye, kubwagwa kwenye
kinyang’anyiro cha ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya
Hanang’ mkoani Arusha mwanasiasa huyo sasa ametangaza vita na Waziri Mkuu
mwenzake mstaafu, Edward Lowassa.
Sumaye ambaye hajatangaza rasmi kuwania kiti hicho, anatarajiwa kupasua jibu
wakati wowote kuanzia leo kueleza kilichotokea; msimamo wake na kwamba yuko
tayari kuwania urais mwaka 2015 endapo Lowassa atawania kiti hicho.
Sumaye aliangushwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na
Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, katika kuwania nafasi ya ujumbe wa NEC wilaya ya
Hanang, matokeo ambayo anaamini yana mkono wa Lowassa.
Chanzo cha karibu na Sumaye, kilisema kuwa pamoja na Waziri Mkuu huyo mstaafu
kushindwa na Dk. Nagu kwa zaidi ya kura 167, amepokea matokeo hayo kwa shingo
upande kwa kile alichoeleza kuwa ushindi huo ni wa mafisadi.
“Hataki kuzungumza chochote leo ila atazungumza nanyi wakati wowote kuanzia
leo, lakini anasema ikiwa Lowassa atawania urais, Sumaye ataingia katika
mpambano huo kukabiliana naye kwa njia yoyote. Hataki kusema ataingia kwa CCM au
chama gani au mgombea binafsi,” anaeleza mtu wa karibu na Sumaye.
Vyanzo vilivyo karibu na mwanasiasa huyo vimeeleza kuwa tayari Sumaye
amefanya mazungumzo na baadhi ya wanasiasa wenye ushawishi wanaojipambanua kama
wapiganaji wa ufisadi ili kuunganisha nguvu kwa ajili ya kukabiliana na kambi ya
Lowassa.
Mbali ya kundi la Sumaye na wanasiasa wengine kuanza mkakati huo, wapo pia
wanasiasa wengine wenye majina makubwa ndani ya chama, serikali na wastaafu
wanaotajwa kuingia kwenye muungano huo.
Akijibu tuhuma hizo kwa kifupi, Lowassa alisema endapo Sumaye ataitisha
mkutano na waandishi wa habari na kutoa tuhuma hizo, nitajibu.
Hata hivyo, baadhi ya wafuasi wa Sumaye na watendaji wa ndani ya serikali
wamesema kuanguka kwa mwanasiasa huyo mkongwe katika uchaguzi wa wilaya
kunamuweka vizuri zaidi kisiasa kutokana na mazingira tete ya kisiasa ndani ya
CCM, chama ambacho kimechokwa na umma.
Waziri wa zamani wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) na mbunge wa zamani wa
jimbo la Makete, Dk. Hassy Kitine, alikaririwa juzi akisema kuwa kuangushwa kwa
Sumaye katika nafasi ya NEC hakuwezi kumuathiri kisiasa kama atachukua uamuzi wa
kuwania urais mwaka 2015 kupitia CCM.
Dk. Kitine alitoa kauli hiyo alipoombwa na gazeti moja kutoa maoni yake juu
ya matokeo ya NEC wilayani Hanang’ kama yana athari kwa mustakabali wa kisiasa
kwa kiongozi huyo.
“Katiba ya CCM haina kipengele kinachosema kama unataka kuwania urais ni
lazima uwe mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM , kwa hiyo nasema kama kweli Sumaye
anatafuta urais bado ana nafasi ya kuwania nafasi hiyo,” alikaririwa akisema Dk.
Kitine.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, naye alimtia moyo
Sumaye kwa kuweka bayana kuwa uchaguzi wa NEC ni wa ngazi ya wilaya tu kwa hiyo
Sumaye anaweza kuwa anakubalika kitaifa kuliko katika wilaya anayotoka huku
akitumia usemi kwamba ‘nabii hakubaliki kwao’.
Katika hatua nyingine, hali inaelezwa kuwa tete ndani ya CCM baada ya kuwapo
kwa taarifa za ushangiliaji kutoka kwa wafuasi na viongozi wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao wameona wanazidi kusafishiwa njia.
“CHADEMA wameshangilia sana kwa kuwa sasa jimbo hilo litachukuliwa kirahisi.
Walikuwa wanamuogopa Sumaye na kumheshimu hivyo kwa sasa watu wake wote
wanahamia CHADEMA.
“Wanasema mafisadi walihakikisha wanampa kila mjumbe kiwango cha chini kabisa
cha shilingi 100,000 kumuangusha Sumaye. Uongozi wote wa CCM wa wilaya na hata
baadhi kwenye mkoa walijipanga kumuangusha,” anasema.
Katika uchaguzi huo wa Hanang, hali ilianza kuwa tete toka hatua za awali,
ambapo Dk. Nagu alitajwa kushinikiza kubadilishwa kwa muhtasari wa kikao cha
wilaya kilichokata jina lake na hivyo kurudishwa tena.
Taarifa kutoka Hanang zinaeleza kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU), ilifanya kazi katika mazingira ya aibu kutokana na kuonekana
kufumbia macho vitendo vya rushwa iliyogawiwa waziwazi.
Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah, alinukuliwa
akisema kwamba taasisi yake inafuatilia kwa karibu uchaguzi huo ndani ya CCM ili
kubaini watu wanaotumia rushwa, kauli ambayo imeelezwa kuwa ya kisiasa
zaidi.
Dk. Hoseah alitoa kauli hiyo akijibu hoja mbalimbali za washiriki wa
kongamano la kujadili utekelezaji wa awamu ya pili ya mpango wa kupambana na
rushwa nchini na mapendekezo yanayopaswa kuzingatiwa katika utekelezaji wa
mpango wa awamu ya tatu (2012 – 2016).
Uchaguzi huo ulifanyika siku chache baada ya CCM kupitisha majina ya
walioomba nafasi hizo huku wanachama wengi wakienguliwa kutokana na kukosa sifa
katika kikao kilichomalizika mjini Dodoma mapema wiki hii.
Katika hatua nyingine, Lowassa ametamba kuwa wananchi wa Monduli ndiyo msuli
wake wa kisiasa.
Akizungumza baada ya ushindi wa NEC alioupata, Lowassa alisema ushindi huo
mkubwa umedhihirisha kuwa ana misuli ya kisiasa kwa wananchi wake.
“Kuna mzee rafiki yangu aliniambia kuwa katika kazi za siasa angalia ‘grass
roots’, watu wanakuwa ndiyo msuli wako kisiasa, na mimi watu wa Monduli ndiyo
msuli wangu,” alisema Lowassa ambaye anatajwa kuwa mmoja wa watu watakaowania
urais mwaka 2015.
“Wananchi wa Monduli mmenithibitishia hilo na nawashukuru sana kutoka kwenye
sakafu ya moyo wangu, jibu la thibitisho hilo kwangu ni utumishi uliotukuka
kwenu,” aliongeza.
Lowassa alipata asilimia 93 ya kura dhidi ya wapinzani wake, Dk. Sulesh Toure
aliyetangaza kujitoa baada ya kuona upepo mbaya kwake na Nanai Konina
Na Martin Malera TANZANIA DAIMA
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=41145
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=41145
No comments:
Post a Comment