MBUNGE wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Kabwe ameiandikia barua Ofisi ya Bunge kuitaarifu nia yake ya kuwasilisha
hoja binafsi katika Mkutano wa 11 wa Bunge kuliomba liazimie Serikali iwasiliane
na taasisi za kimataifa, hasa benki kusaidia kurejeshwa nchini fedha zote haramu
ambazo zimefichwa na Watanzania katika benki za nchini Switzerland na kwingineko
duniani.
Taarifa zilizopatikana jana
kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni zimeeleza kuwa Zitto anaomba Serikali
ifanye hivyo kwa Benki ya Dunia kupitia taasisi yake ya Stolen Asset Recovery
Initiative, kutekeleza jukumu hilo.
Taarifa hizo zimeeleza kuwa
katika barua hiyo Zitto anatumia kifungu cha kanuni za bunge namba 55 (1) na
(2), na hoja yake itaainisha fedha ambazo Benki ya Taifa ya Switzerland
ilitangaza kwamba Watanzania wamezihifadhi, ambazo ni Sh297
bilioni.
Barua hiyo imeainisha kuwa
fedha hizo ni sawa na Dola za Marekani 186 milioni na Zitto amebainisha kuwa
hoja yake hiyo itaainisha namna na njia ambazo zilitumika kutorosha fedha hizo
kwenda katika benki hiyo na nyingine za nje.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas
Kashillilah alikataa kuthibitisha kupokea barua hiyo badala yake alieleza kuwa
hilo ni suala la kiofisi.
"Ni suala la ndani la
ofisi, siwezi kueleza kama ni kweli nimepokea au la, isipokuwa suala hilo
linafahamika na ofisi ya Bunge ililipokea alipoliwasilisha bungeni hivyo
linafanyiwa kazi," alisema Kashillilah.
Mapema mwaka huu, baadhi ya
vyombo vya habari likiwamo gazeti hili, vilifichua kuwapo kwa fedha zilizofichwa
nchini Uswisi na baadaye ilibainika kwamba fedha hizo ni mali ya Watanzania 27
wakiwamo wanasiasa na wafanyabiashara.
Gazeti hili pia lilibaini
kwamba mmoja wa walioficha fedha hizo anamiliki Dola za Marekani milioni 56
(sawa na Sh89.6 bilioni).
Katika uchunguzi wake,
Mwananchi limebaini pia kuwa kiasi cha fedha kilichothibitishwa kumilikiwa na
Watanzania hao ni jumla ya Dola za Marekani 186 milioni (takriban Sh300 bilioni)
kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1600 kwa Dola ya
Marekani.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa
mbali na kigogo anayemiliki Sh90 bilioni, wapo wengine wanne, ambapo anayefuatia
anamiliki Dola 30 milioni (Sh48 bilioni), mwingine Dola 20 milioni (Sh32
bilioni) na wengine wawili kila mmoja anamiliki Dola 10 milioni (Sh16
bilioni).
Kwa kuangalia fedha hizo ni
dhahiri kwamba vigogo watano tu kati ya kundi la Watanzania 27, wanamiliki Dola
126 milioni (Sh201.6 bilioni) sawa na asilimia 67.74 ya fedha hizo, wakati
wengine 22 waliobaki wanamiliki Dola 60 milioni (Sh96 bilioni) sawa na asilimia
32.25.
Habari hizo zilikuwa
zikinukuu taarifa ya Benki Kuu ya Uswisi iliyoitoa na kuonyesha kuwapo kwa kiasi
cha Sh315.5 bilioni zilizotoroshwa Tanzania na kufichwa nchini humo na vigogo
ambao ni wanasiasa pamoja na wafanyabiashara.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment