UTANGULIZI:
Kwa nyakati mbalimbali kumekuwepo na mijadala kwenye mitandao ya
kijamii kuhusu utendaji kazi wangu katika kuwezesha maendeleo Jimboni Ubungo.
Mijadala hiyo imeshika kasi jana tarehe 20 Agosti 2012 siku nzima baada ya
habari kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti la Tanzania Daima “Mnyika kinara
bungeni” ambayo imerejea rekodi za bunge na kuniweka katika orodha ya
wachangiaji wa mara kwa mara bungeni.
Napokea kwa unyenyekevu pongezi zilizotolewa na wachangiaji
mbalimbali lakini izingatiwe kuwa michango yangu bungeni ni matokeo ya heshima
mliyonipa ya kuwawakilisha. Aidha yapo maoni machache ambayo yametoa tafsiri
tenge kuhusu kazi ya mbunge na wengine mmetaka nieleze nimefanya kazi gani za
maendeleo jimboni Ubungo.
Tarehe kama ya leo 21 Agosti 2005 nilianza mchakato wa kuwa kugombea
ubunge nikiwa kwenye chakula na watoto yatima, tarehe kama hiyo mwaka 2010
nilianza kampeni za uchaguzi mitaani Ubungo, tarehe hii hii kwa mwaka huu wa
2012 naomba niitumie kutoa taarifa fupi ya utekelezaji kwa masuala ya maendeleo
katika mwaka wa fedha 2011/2012 uliomalizika tarehe 30 Juni 2012; taarifa ya
kina ya utekelezaji nitaitoa nitakapotimiza miaka miwili ya
utendaji.
AHADI NILIZOTOA WAKATI WA UCHAGUZI WA MWAKA
2010
Kabla ya kueleza kazi nilizofanya katika kutimiza majukumu ya kibunge
katika kuwezesha maendeleo jimboni ni muhimu nikawapa rejea ya ahadi nilizotoa
wakati wa uchaguzi wa mwaka 2010 ili kupata msingi wa kupima
utekelezaji.
Wakati wa kampeni nilitoa ahadi chache na kuelekea mwishoni mwa
kampeni niliorodhesha ahadi zote na kuziweka kwenye maandishi ikiwa ni mkataba
kati ya mbunge na wananchi wa kutumika kama rejea katika kipindi cha miaka
mitano ya utumishi 2010 mpaka 2015.
Ahadi hizo ziko katika kipeperushi cha AMUA ambacho tulikisambaza
kwenye kaya mbalimbali jimboni wakati wa kampeni, ahadi hizo nilizirudia mara
baada ya kuchaguliwa na zinapatikana hapa: http://mnyika.blogspot.com/2010/11/ujumbe-wa-mbunge-shukrani-twende-kazi.html
UTEKELEZAJI KATIKA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA NA
NUSU
Toka kuapishwa mwezi Novemba 2010 mpaka mwezi Juni 2012 ni takribani
mwaka mmoja na na miezi tisa ya kuwatumikia wananchi wa Ubungo kwa nafasi
niliyochaguliwa ya mbunge wa Ubungo; hizi ni baadhi katika orodha ya za
maendeleo ambazo nimeshiriki jimboni:
ELIMU:
Akili na vipaji ambavyo kila mwanadamu amejaliwa ndiyo mtaji mkuu wa
kujikwamua kimaisha. Katika muktadha huo katika kipindi husika nimesimamia
yafuatayo kuwezesha elimu bora:
Mbunge amefuatilia kupitia vikao vya manispaa ya Kinondoni na kupitia
ziara jimboni, maswali bungeni ili kuhakikisha ruzuku ya bajeti ya elimu kwa
wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari, inafika na kuboresha upatikanaji wa
vifaa vya elimu na huduma zingine za muhimu katika Jimbo la Ubungo, katika mwaka
2012/2013 nitafuatilia kwa karibu zaidi kasoro zilizobainika katika mwaka
2011/2012 .
Katika kipindi husika mbunge ameendelea kutetea haki na maslahi ya
walimu na wanafunzi wakiwemo wa elimu ya juu wa Jimbo la Ubungo. Aidha,
nimeshiriki katika kuwezesha uamuzi wa kuhamisha fedha katika mafungu mengine
yasiyokuwa ya lazima kuelekeza katika matengenezo ya madawati kwa shule za
msingi na sekondari ambapo zaidi ya madawati 7,000 yamesambazwa katika Jimbo la
Ubungo kutoka Manispaa ya Kinondoni, Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) na
kutoka Sekta Binafsi. Kwa ushirikiano na madiwani tumefuatilia kuhakikisha mgawo
wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na vyoo katika shule za msingi na
sekondari katika kata mbalimbali kutoka katika Manispaa ya Kinondoni na Mfuko wa
Maendeleo ya Jimbo (CDCF), orodha ya shule na viwango vya fedha vilivyotumika
inaweza kupatikana katika Ofisi ya Mbunge.
Mbunge amependekeza sehemu ya fedha za mfuko wa kuchochea maendeleo
ya jimbo (CDCF) kutumika kutoa elimu maalum ya kuwawezesha wananchi kujua haki
zao, fursa zilizopo na namna ya kujiendeleza, haswa kwa akina mama, vijana na
walemavu. Mfano; haki za mirathi kwa wajane na kukuza vipaji kwa vijana. Hata
hivyo, utekelezaji wa kazi hii haukuwezekana kwa kutumia CDCF kwenye mwaka wa
fedha 2011/2012 kutokana na utata kuhusu tafsiri ya shughuli za kuchochea
maendeleo zinazoweza kutengewa fedha kutoka kwenye mfuko, hivyo shughuli hiyo
itazingatiwa kwa ukamilifu kwenye mwaka wa fedha 2012/2013 baada ya kibali
kupatikana.
Ili kuziba pengo nje ya CDCF katika mwaka 2011/2012 kupitia ofisi ya
mbunge Ubungo na Asasi ya Maendeleo Ubungo (UDI) tumefanya programu ya “Toa
Kitabu Kisomwe” na pia kuunganisha vijana na wanawake na elimu maalum kupitia
taasisi zingine.
Mbunge amechangia asilimia 20 (20%) ya mshahara wake kwa
mwezi kwenye masuala mbalimbali ya elimu, orodha ya baadhi ya michango kwa
shughuli za elimu kwa wanafunzi na walimu wa msingi, sekondari na vyuo inaweza
kurejewa katika Ofisi ya Mbunge (majina ya waliopewa michango yamehifadhiwa
kulinda faragha).
Kazi hizi zitapanuliwa zaidi katika mwaka wa fedha 2012/2013 kupitia
Mfuko wa Elimu Ubungo tutakaouzindua karibuni.
AJIRA:
Katika kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa vijana na wanawake kuweza
kujiajiri mbunge alifanikiwa kushawishi Manispaa ya Kinondoni kuongeza fedha za
mikopo kwa vikundi vya kina mama na vijana ambapo awali zilikuwa zikitengwa
milioni 20 tu, na hivyo milioni zaidi ya 200.
Orodha ya vikundi vilivyopatiwa mikopo na mitaji mpaka sasa katika
Jimbo la Ubungo inapatikana kwenye Ofisi ya Mbunge. Aidha, mbunge ametetea
wafanyabiashara wadogo kuendelea kutengewa maeneo ya biashara na katika mwaka
2011/2012 amewezesha kamati maalum inayohusisha wafanyabiashara na Manispaa
kuundwa kwa ajili ya kuwezesha wafanyabiashara wa Ubungo kupatiwa maeneo katika
masoko yaliyotengwa. Katika mwaka 2012/2013 hatua zitaendelea kuchukuliwa kwa
ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo ambao hawajapata maeneo mpaka
sasa.
Mbunge amefanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha nguo cha Urafiki
ili kuzungumza na wafanyakazi na menejimenti katika kuisimamia serikali
kushughulikia matatizo yaliyojitokeza katika kiwanda na kuathiri ajira na ujira
bora. Matokeo ya ziara ya mbunge na ufuatiliaji bungeni yamefanya kiwanda hicho
kutembelewa pia na kamati ya bunge na mawaziri husika ambapo hatua zimeanza
kuchukuliwa, katika mwaka wa fedha 2012/2013. Mbunge ataendelea kufuatilia kwa
karibu matatizo yanayoendelea kuhusu ufisadi na uwekezaji katika kiwanda
husika.
Aidha, mbunge amefuatilia pia masuala ya ajira katika viwanda
vilivyofunguliwa kwenye maeneo ya uwekezaji wa kiuchumi (EPZ/SEZ) yaliyopo
katika jimbo la Ubungo ikiwemo kutaka kutengwa kwa maeneo maalum ya wawekezaji
wadogo.
Katika kupanua wigo wa ajira mbunge amefuatilia pia kuhusu viwanda
vingine vilivyobinafsishwa au kuuzwa miaka ya nyuma katika Jimbo la Ubungo
mathalani Ubungo Garments; Ubungo Spinning Mill; Polysacks Ltd; Tanzania
Sewing Thread; Coastal Diaries (Maziwa) na Kiwanda cha Zana za Kilimo (UFI); na
hatimaye serikali imemjibu kuwa waraka utawasilishwa kwenye baraza la mawaziri
ili kurejesha viwanda vilivyodidimizwa kinyume cha masharti ya mikataba. Katika
utekelezaji wa hatua hiyo, mbunge amependekeza kuwa miongoni mwa maeneo ya
viwanda yatakayorejeshwa kutengwe eneo maalum kwa ajili ya wenye viwanda vidogo
vidogo katika jimbo la Ubungo ili kupanua wigo wa ajira hususan kwa vijana
katika mwaka wa fedha 2012/2013.
Mbunge ameunga mkono jimboni na ndani ya bunge madai ya ujira bora na
stahili za wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi kama walimu,
madaktari/manesi, polisi, madereva nk. Hata baada ya nyongeza ndogo ya mishahara
iliyopatikana kufuatia shinikizo la migomo kutoka vyama vya wafanyakazi, mbunge
ataendelea kuungana na wafanyakazi na wabunge wengine katika kutaka kuboreshwa
kwa maslahi ya wafanyakazi na mazingira ya utoaji huduma hususan katika sekta za
elimu, afya, usalama na mahakama. Katika ya masuala ambayo aliyapata kipaumbele
katika mwaka wa fedha 2011/2012 ni nyongeza ya posho ya lishe (rationing
allowance) kwa askari polisi kutoka laki moja mpaka laki moja unusu suala ambalo
serikali imelitekeleza katika bajeti ya mwaka wa fedha
2012/2013.
MIUNDO MBINU:
Msimamo wangu katika kipindi chote umekuwa kwamba pamoja kuunga mkono
uwekezaji kwenye upanuzi wa barabara kuu, ujenzi wa miundombinu ya mradi wa
mabasi yaendayo haraka na ujenzi wa fly overs, miradi hii kwa ujumla wake
iliyotengewa zaidi ya bilioni 240 inachukua muda wa kati na muda mrefu hivyo
kukamilika kwake ni mpaka mwaka 2015 au zaidi. Hivyo ili kupunguza msongamano
katika barabara kuu ya Morogoro, pamoja na mbinu zingine mbunge amekuwa mstari
wa mbele kutaka barabara za pembezoni zijengwe kwa haraka; hatimaye baada ya
ufuatiliaji wa mara kwa mara kupitia ziara jimboni, vikao vya manispaa, vikao
vya bodi ya barabara, ziara jimboni, mawasiliano kwa barua na mamlaka husika na
kuhoji bungeni Serikali imekubaliana na mapendekezo tuliyowasilisha hivyo
maamuzi yamefikiwa kuwa barabara husika zihudumiwe na Serikali kuu (TANROADS)
badala ya Manispaa.
Jumla ya shilingi bilioni 10.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa
barabara zifuatazo: Mbezi Luis kupitia Goba mpaka Mbezi Tangi Bovu; Mbezi kwa
Yusuph- Msakuzi- Mpiji Magohe mpaka Tegeta/Bunju; Mbezi-Malambamawili-Kinyerezi,
Kimara-Mavurunza-Bonyokwa; Ubungo Maziwa-External,
Kimara-Kilungule-Makoka-Makuburi, Kimara-Matosa-Mbezi; Ubungo-Msewe-Chuo Kikuu
na nyingine katika maeneo mengine.
Katika mwaka wa fedha 2012/2013 Mbunge ataendelea kuisimamia serikali
ili itenge bilioni 100 kujenga kwa kiwango cha lami barabara tajwa za pembezoni
za kupunguza msongamano haraka zaidi na pia kuboresha usafiri wa maeneo ya
pembezoni kwa kuwa baadhi ya barabara hizo zilitengenezwa kwa kiwango cha
changarawe kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 lakini zimeharibika tena baada ya
mvua zilizonyesha katika jiji la Dar es salaam.
Katika mwaka wa fedha 2011/2012 tumefuatilia madaraja mbalimbali
kujengwa ikiwemo Daraja Golani, Msewe, Matosa nk pia kupitia mfuko wa maendeleo
ya Jimbo (CDCF) vivuko kwa watembea kwa miguu vimejengwa Makurumla na Msigani;
orodha zaidi ya matengenezo ya barabara yaliyofanyika inaweza kurejewa katika
Ofisi ya Mbunge.
Kufuatia ufuatiliaji wa karibu kwa njia mbalimbali hatua imechukuliwa
ya kupeleka umeme katika eneo la Goba Matosa (hata hivyo bado kuna malalamiko ya
eneo lilirukwa la Mgeni Chongo) ambalo tunaendelea
kufuatilia.
Aidha, miradi iliyokuwa imekwama kwa muda mrefu ya kupeleka umeme
katika miradi ya maji ya King’ongo na Kilungule inaendelea kutekelezwa kwa
haraka zaidi. Mbunge amefuatilia mara kwa mara ahadi ya Rais ya kupunguzwa kwa
gharama za umeme na hatimaye ahadi imetolewa ya utekelezaji kuanza kuanzia
Januari 2013, pia kanuni za Februari 2011 zimetungwa kuhusu kurejeshwa kwa
gharama kwa wateja wanaolazimika kuvuta umeme zaidi ya umbali wa
kawaida.
Katika mwaka 2012/2013 mbunge ataendelea kuisimamia serikali
kurekebisha kanuni hizo kwa kuwa zina vifungu visivyotekelezeka na kutaka pia
gharama za nguzo na nyinginezo ziwekwe kwenye bili ya mteja kama umeme
uliolipiwa kabla. Orodha ya maeneo mengine katika Jimbo la Ubungo ambayo
ufuatiliaji umefanyika kuhusu kusambaziwa umeme inapatikana katika Ofisi ya
Mbunge.
MAJI:
Katika kufuatilia masuala ya maji nilianza kwa kufanya Kongamano la
Maji katika Jimbo la Ubungo mwanzoni mwa mwaka 2011 ili kuwakutanisha wananchi,
mamlaka husika na wadau wengine katika kuunganisha nguvu kupata
ufumbuzi.
Hatua nyingine zote nilizochukua baada ya hapo zilikuwa ni za
ufuatiliaji kuwezesha utekelezaji wa haraka. Nikiri kwamba katika hatua za awali
ushirikiano kutoka DAWASA, DAWASCO na Wizara ya Maji ulikuwa mdogo kwa kiwango
cha kuamua kuwaunganisha wananchi kupitia ‘maandamano ya maji’ kwenda DAWASCO.
Toka wakati huo ushirikiano umeongezeka kwa upande wa DAWASCO ambapo
nimeshafanya nao ziara ya kikazi ya kata mbalimbali ya kutembelea maeneo yenye
matatizo na hatua zimechukuliwa ambazo zimewezesha baadhi ya maeneo kuanza
kutoka maji.
Pia, wakati wa hatua hizo nimewaonyesha DAWASCO biashara haramu ya
maji iliyokuwa ikiendelea na baadhi ya maeneo wamechukua hatua ikiwemo kwa
watendaji wao. Hata hivyo, udhaifu wa kimfumo uliopo ni mkubwa kuliko hatua
ambazo zimeweza kuchukuliwa mpaka sasa. Katika mazingira hayo nilianza pia
kutaka hatua za DAWASA na tayari nao nimefanya nao ziara ya kikazi kwenye vyanzo
vya maji pamoja na matenki ya maji, na kutaka hatua za haraka za ushirikiano
kati ya DAWASA na DAWASCO.
Kwa maana ya miradi ya muda mrefu ya mwaka 2013/2014 kumetengwa fedha
kuanzia mwaka 2012/2013 zaidi ya bilioni 200 kutokana na fedha za MCC na Mkopo
wa India kwa ajili ya upanuzi wa vyanzo vya Ruvu Juu na Ruvu Chini, ujenzi wa
Bwawa la Kidunda na ujenzi wa mabomba mengine miradi ambayo itagusa wananchi wa
Ubungo. Hata hivyo, hatua hizi za muda mrefu hazileti matumaini bila hatua za
haraka ambazo zilipaswa kuchukuliwa katika mwaka wa fedha
2011/2012.
Katika kuwezesha hatua za haraka kwa mwaka wa fedha 2011/2012
nilifuatilia ratiba ya mgawo wa maji kuweza kutolewa kwa mbunge na kwa ngazi za
kata na mitaa na kufuatiliwa ili mgawo uwezeshe kuheshimiwa bila ya upendeleo wa
baadhi ya maeneo au hujuma kwa ajili ya kuwezesha biashara haramu ya maji. Ofisi
ya mbunge wakati wote imetaka kupatiwa taarifa pale mamlaka husika au ngazi
tajwa zinaposhindwa kufuatilia ratiba husika ili kuweza kuingilia kati. Kuanza
kuweka miundombinu ya maji katika maeneo yaliyorukwa kwenye awamu ya kwanza ya
uwekaji wa mabomba, tayari utekelezaji umeshaanza katika maeneo ya Mbezi na
maeneo mengine utafanyika kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2013 kwa mujibu wa ahadi
zilizotolewa na DAWASCO/DAWASA kwa mbunge.
Katika kutekeleza ahadi ya kuhamasisha ujenzi wa visima kwenye maeneo
ambayo hayafikiki kirahisi na mtandao wa maji ya bomba kama suluhisho la muda,
huku tukifuatilia ufumbuzi wa kudumu katika maeneo hayo, mbunge amefuatilia
uchimbaji wa visima uliokuwa umesimama katika maeneo ya Mavurunza/Bonyokwa,
Kilungule na King’ongo kwa kwenda maeneo husika, kuziandikia mamlaka
zinazohusika na kuhoji kwenye vikao vya manispaa, bungeni na kufanya ziara za
ukaguzi wa maendeleo ya miradi.
Uzinduzi kwa miradi ya Mburahati ulifanyika mwanzoni mwa mwaka 2011
na hatimaye sasa uzinduzi wa maeneo yaliyotajwa utafanyika katika mwaka huu wa
2012 kwa kuratibiwa na DAWASA na Wizara ya Maji.
Aidha, uchimbaji wa visima kama hivyo unaendelea katika maeneo ya
Saranga na Malambamawili. Aidha, kupitia miradi ya Manispaa ikiwemo mradi
unaofadhiliwa na benki ya dunia mbunge amefuatilia uchimbaji katika maeneo ya
Mpiji Magohe, Msakuzi, Makoka na Msumi ambao unasuasua kutokana na udhaifu wa
kiutendaji.
Mbunge ameunga mkono jitihada zinazofanywa na wadau wengine wa
maendeleo Jimboni Ubungo katika masuala ya maji hususani Shirika la Kibelgiji
(BTC) katika maeneo ya Kwembe na Kibamba na amewasiliana na DAWASA/DAWASCO kwa
ajili ya hatua za kusaidia miradi husika na TANESCO kwa upande wa kuweka
transfoma yenye uwezo mkubwa zaidi ili kuwezesha pampu za maji kwenye maeneo
husika ziweze kufungwa. Orodha ya maeneo mengine yaliyochimbwa visima vidogo
ipo katika Ofisi ya Mbunge.
Mbunge amefanikiwa kufanya suala la maji kuwa moja ya masuala
yanayojadiliwa mara kwa mara kwenye vikao vya Manispaa ya Kinondoni hali ambayo
haikuwepo kabla. Aidha alipendeza na hatimaye ukafanyika ufuatiliaji wa miradi
iliyo chini ya jamii au mamlaka za ngazi ya chini iliyokwama kwa muda mrefu na
hivyo kukosesha wananchi maji katika maeneo mbalimbali ambayo hayapewi huduma ya
moja kwa moja na DAWASA/DAWASCO. Kati ya miradi hiyo baadhi imefufuliwa kama wa
Msewe Golani na mingi inaendelea kusuasua ikiwemo ya kata ya Goba. Mbunge
amependekeza kwa DAWASA kwamba maeneo ambayo hayakuwa yakihudumiwa na DAWASCO
ikiwemo ya kata ya Goba yachukuliwe moja kwa moja na mamlaka husika kwa kuwa
kutokana na ongezeko la watu maeneo hayo hayawezi kuhudumiwa kwa ufanisi na
kamati za maji kama ilivyokuwa miaka ya zamani.
Mbunge amefuatilia pia masuala ya bei na ubora wa maji na kuitaka bei
ya maji inayotozwa kwenye Viosk inaendana na viwango vilivyopangwa na mamlaka
husika (EWURA), kufuatia hatua hizo operesheni zimefanyika katika maeneo ambayo
yanatoza maji kinyume na bei iliyotangazwa na DAWASCO imeingia mikataba na
waendeshaji wa vioski husika kuhusu bei elekezi. Hata hivyo, changamoto
imeendelea kuwa ni usimamizi wa utawala wa sheria katika kuhakikisha bei
inayotozwa ni ile inayopaswa kutoswa kwa mujibu wa maagizo ya EWURA. Katika
kipindi husika mbunge ametaka pia EWURA itoe bei elekezi kwa upande wa maji
katika jiji la Dar es salaam kwa upande wa sekta binafsi ili kudhibiti pia
biashara holela ya maji ya kwenye malori. Katika mwaka wa fedha 2011/2012 EWURA
iliahidi kutoa kanuni za kudhibiti biashara husika hatua ambayo mpaka sasa
haijachukuliwa, suala ambalo mbunge atalifuatilia katika mwaka wa fedha
2012/2013.
UWAJIBIKAJI:
Mbunge amekuwa mstari wa mbele katika kupambana na ufisadi na
matumizi mabaya ya fedha ngazi mbalimbali ili kuchangia katika kuhakikisha
fedha nyingi zinazopatikana kila mwaka zinatumika kuwahudumia wananchi, ikiwemo
kwa kutaka kushughulikiwa kwa mapungufu yaliyoanishwa na wakaguzi wa hesabu
katika vipindi vilivyopita. Mathalani mbunge amefuatilia utekelezaji wa
mapendekezo ya Ukaguzi Maalum (Special Audit) ya Kituo cha Mabasi cha Ubungo
uliofanyika mwaka 2009 lakini utekelezaji wa matokeo ulikuwa ukisuasua. Alifanya
hivyo kupitia bungeni na katika vikao vya halmashauri ya Jiji la Dar es salaam
na hatimaye baadhi ya mapendekezo yametekelezwa ikiwemo kumwondoa mkandarasi
aliyekuwa akikusanya mapato chini ya kiwango; aidha mbunge ataendelea kufuatilia
mapendekezo mengine kuhusu mikataba mibovu iliyoingiwa katika kituo
husika.
Mbunge amefanya hivyo vile vile kuhusu vitega uchumi vingine vya Jiji
la Dar es salaam ikiwemo Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA). Aidha, kwa
kushirikiana na madiwani amefuatilia pia miradi hewa au ya chini ya kiwango
iliyofanyika katika miundombinu, elimu na maji na hatua mbalimbali zimechukuliwa
kama zinavyoelezwa katika Taarifa za Ofisi ya Mbunge.
Mbunge kupitia uwakilishi bungeni na kupitia hatua zingine nje ya
bunge amezifuatilia mamlaka za serikali kuhusu masuala mbalimbali yanayowagusa
wananchi wa Ubungo, mathalani EWURA katika nishati/mafuta, SUMATRA katika
usafiri na TANESCO katika umeme.
Katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge atafanya ziara za kikazi
pamoja na mamlaka husika katika maeneo mbalimbali yenye kero ili kuziwezesha
kuendelea kuchukua hatua zaidi kuhusu maeneo hayo kwa ajili ya kuchangia katika
maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla.
Mbunge amefanya mikutano na wananchi katika kata zote 14 za Jimbo la
Ubungo kwenye maeneo mbalimbali ya kiserikali na ya kichama kwa ajili ya
kutimiza wajibu wa uwakilishi kabla na baada ya vikao vya
bunge.
Aidha mbunge ameshiriki katika mikutano ya wakazi ya masuala ya
maendeleo jimboni kama ambavyo imetajwa katika Taarifa ya Utendaji. Mbunge
amewezesha ofisi ya mbunge kuwa vitendea kazi pamoja na wasaidizi wawili wakati
wote baada ya kukwama kupata vifaa kutoka kwenye mfumo wa kawaida wa
kiserikali.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2011/2012 maombi ya mbunge kupata ofisi
ya kutumia jimboni kutoka kwenye majengo ya manispaa au ya wilaya yalikataliwa
na katika mwaka 2012/2013 mbunge ataweka mkazo katika kufuatilia eneo kwa ajili
ya ujenzi wa ofisi ya mbunge.
Aidha, mbunge amewajibika katika kuisimamia serikali bungeni na
kushiriki katika kutunga sheria. Rejea katika ofisi ya Mbunge kuhusu kazi za
mbunge bungeni inaeleza masuala ambayo mbunge ameisimamia serikali bungeni,
hatua zilizochukuliwa na serikali kupitia mchango wake na pia sheria ambazo
amewasilisha majedwali ya marekebisho katika vifungu mbalimbali vilivyokubaliwa
na vilivyokataliwa.
USALAMA:
Mbunge amechangia katika harambee ya ujenzi wa Kituo cha Polisi
Mavurunza ambapo vifaa vya awali vilichangiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo
(CDCF) lakini pia fedha taslimu zilichangwa na mbunge kutoka mfuko wake binafsi.
Aidha, kupitia CDCF mbunge amechangia pia kwenye ujenzi wa Kituo kidogo cha
Polisi Golani Msewe na pia kituo cha Polisi Kata ya
Sinza.
Pia, mbunge ameanza ufuatiliaji wa ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kimara katika eneo lenye nafasi tofauti na eneo la sasa la barabarani la Mbezi kwa Yusuph; kufuatia ufuatiliaji wa mbunge tayari Wizara ya Mambo ya Ndani imeiandikia barua Manispaa ya Kinondoni kuomba eneo.
Kadhalika, mbunge amefuatilia kuhusu eneo la ujenzi wa kituo cha
Polisi kata ya Goba ambapo kwa mujibu wa taarifa toka ngazi ya kata eneo
limekwishapatikana. Katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge ataweka kipaumbele
katika kazi ambazo zilianza kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 ili ziweze
kukamilika.
Mbunge ameshirikiana na polisi na viongozi wa kata/mitaa kufanya
harambee kuhakikisha doria inakuwepo ili kupunguza vitendo vya wizi, ukabaji na
ujambazi hususani kwenye maeneo yenye vitendo vingi vya uhalifu mathalani ya
Kimara B kupitia ulinzi shirikishi na polisi jamii.
Aidha, ili kuwe na mfumo endelevu wa kuhudumia vikundi vya ulinzi
shirikishi mbunge alipendekeza kwamba masuala ya ulinzi na usalama kuwa sehemu
ya vipaumbele vya maendeleo katika mapato ya ndani ya Manispaa kama ilivyo kwa
sekta za elimu, afya, barabara nk. Kwa usimamizi wa Meya pendekezo hilo
liliingizwa kwenye baraza la madawani na kutakiwa kutekelezwa kupitia fedha
zinazobaki katika kata kutokana na ufanisi katika makusanyo ya ndani ili
kuimarisha ulinzi na usalama.
AFYA:
Mbunge aliguswa na kasi ya kupungua kwa fedha za wahisani katika
bajeti ya afya kwa masuala ya matibabu kwa wanaoishi na UKIMWI/VVU, Wazee,
Walemavu na wagonjwa wa kifua kikuu, hivyo pamoja na kuhoji bungeni na kutaka
nyongeza ya bajeti kwenye Wizara ya Afya amechukua hatua jimboni kwenye ngazi ya
Manispaa kwa kupendekeza kiwango cha fedha toka vyanzo vya ndani kuongezwa hatua
ambayo imeanza kuchukuliwa kwa ajili ya mwaka wa fedha
2012/2013.
Kwa ajili ya afya mazingira mbunge alipendekeza kwamba tathmini
ifanyike kuhusu mfumo mzima wa uzoaji taka katika kata mbalimbali za Jimbo la
Ubungo na Manispaa ya Kinondoni kwa ujumla kutokana na kukithiri kwa uchafu
katika maeneo mbalimbali. Kufuatia pendekezo hilo Meya alifanya mkutano na
wenyeviti wa mitaa na watendaji wengine ambapo maazimio ya hatua mbalimbali
yalifikiwa ambayo yameboresha uzoaji taka katika maeneo machache. Hata hivyo,
matatizo ya uchafu yameendelea katika maeneo mengi, hivyo katika mwaka wa fedha
2012/2013 mbunge ataendelea kuisimamia serikali kuu na serikali za mitaa katika
kuchukua hatua kubwa zaidi kuhusu udhaifu wa kimfumo ambao ulishababainishwa
tayari unaochangia kasi ndogo ya uzoaji taka ngumu na uondoaji wa maji taka
katika Jiji la Dar es salaam.
ARDHI:
Mbunge amefuatilia kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wa eneo la
Ubungo Maziwa wanapewa fidia stahiki. Aidha, mbunge amefuatilia na hatimaye
fidia imeanza kulipwa kwa wananchi eneo la Riverside wanaopaswa kubomolewa
kupisha njia mbadala ya kwenda Kibangu.
Hata hivyo, suala la fidia ya ardhi kwa upande wa wananchi wa Kwembe
kupitisha ujenzi wa Chuo Kikuu eneo la Mlongazila limekwama kwa Serikali
kuchukua msimamo wa kutoa fidia ya maendelezo/mali pekee. Mbunge anaendelea
kufuatilia suala hilo katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwa kushirikiana na
wananchi waliofungua kesi mahakamani wakati utekelezaji wa mradi ukiendelea. Kwa
upande mwingine, kiasi cha shilingi bilioni 10 kimeweza kutengwa kwa ajili ya
kulipa fidia kwa wananchi wa Ubungo walio karibu na mitambo ya umeme ambao
walikuwa wanadai fidia toka mwaka 2004.
Mbunge amesisitiza kupitia vikao vya Mkoa, halmashauri ya Jiji,
Manispaa na bunge kuhusu haja ya serikali kuweka kipaumbele katika kusimamia
mpangilio mzuri wa makazi na kuhamasisha upimaji wa viwanja ili wananchi wapate
hati na leseni za makazi kwa urahisi na kwa bei nafuu kutokana na matatizo ya
gharama kubwa na ucheleweshaji yaliyoko hivi sasa. Waziri wa Ardhi na Maendeleo
ya Makazi amemjibu mbunge kuwa wizara itawekwa mfumo ili hati iwe inatolewa kwa
haraka katika muda usiozidi miezi sita. Mbunge amefuatilia mradi wa urasimishaji
unaofanywa na Ofisi ya Rais (MKURABITA) katika eneo la Kimara Baruti, aidha
mbunge ametaka elimu kutolewa kwa wananchi na madiwani na watendaji wengine
kuhusu namna fursa za upimaji na urasimamishaji zinavyoweza kutumiwa katika
maeneo yao.
Mbunge amefuatilia vile vile taarifa kuhusu mji wa kiungani
(Sattellite town) ya Luguruni na maeneo jirani ya mji huo na kubaini kasoro kama
zinavyoelezwa katika Taarifa ya Utendaji, aidha Wizara imeahidi kwamba
muendelezaji mwenza wa mji huo amepatikana na kwamba kasoro zinazoendelea
zitarekebishwa.
Mbunge amefuatilia kupitia hoja binafsi na maswali katika manispaa na
bungeni kuhakikisha viwanja vya umma vilivyouzwa kinyume na taratibu na viwanja
vya wazi vilivyovamiwa, vinarejeshwa. Mfano: viwanja vya Makurumla, Sinza,
Ubungo, Makuburi, Mbezi nk. Kufuatia hatua hizo, sehemu ya viwanja hivyo
imejadiliwa kwenye baraza la madiwani la manispaa ya Kinondoni na pia Waziri wa
Ardhi na Maendeleo ya Makazi ametembelea kata ya Sinza na kuweka mabango kwa
ajili ya wahusika kubomoa. Katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge ataendelea
kufuatilia kwa karibu ili ubomoaji uanze.
HITIMISHO:
Nihitimishe kwa kurejea msimamo wangu kuhusu kazi za mbunge ambao
nimekuwa nao miaka mingi kabla ya kuingia kwenye siasa na niliurudia mwanzoni
mwaka 2010 wakati natangaza nia ya kugombea Ubunge:
“Naamini kwamba mbunge (ambaye pia kwa nafasi yake ni diwani katika
halmashauri) ana wajibu katika maeneo makuu manne (kwa kadiri ya umuhimu) katika
kuwezesha maendeleo Jimboni kwake na kwa taifa kwa ujumla:
Mosi; kusikiliza na kuwakilisha wananchi, Pili; kuisimamia na kuiwajibisha serikali na viongozi wake, Tatu; kushiriki katika kutunga sheria, Nne; kuhamasisha upatikanaji wa huduma.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya wabunge wetu hawaweki kipaumbele katika majukumu ya kwanza matatu ambayo ndio msingi wa ubunge wenyewe. Matokeo yake ni matakwa ya wananchi kutokuwakilishwa kikamilifu, ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mikataba mibovu; uwepo wa sheria dhaifu na kutetereka kwa utawala wa sheria na mifumo ya haki masuala ambayo yanakwaza jitihada za maendeleo za wananchi binafsi za taifa kwa ujumla.
Wabunge wengi wanawaza kwamba jukumu kubwa la mbunge ni kutoa bidhaa na huduma kwa wananchi; wakiacha taifa katika lindi la umasikini na kufanya sehemu ya wananchi kujenga mazoea ya kutegemea hisani toka kwa viongozi wa umma na wafadhili wao.
Mwaka 2005 pamoja na majukumu hayo makuu matatu, nilizungumzia suala la mfuko wa maendeleo ya jimbo. Lakini si katika mwelekeo wa mfuko wa sasa uliopitishwa kuwa sheria. Kwa hiyo, wakati nikiunga mkono jukumu la mbunge kuhamasisha maendeleo na kushiriki kwenye shughuli za kijamii, siamini katika mazoea na mfumo wowote unaomfanya mbunge kuwa “mtoa bidhaa na huduma” (mithili ya ATM) kwani unarutubisha ufisadi wa kisiasa na kuhatarisha mwelekeo mzima wa utawala bora. Kama ambavyo siamini pia katika siasa chafu za rushwa, uongo na aina nyingine ya upofu wa kimaadili katika kampeni na uongozi kwa ujumla.
Haiwezekani wakati ambapo makisio yanaonyesha kwamba zaidi ya trilioni mbili (sawa na milioni milioni mbili) zinapotea kila mwaka kupitia misamaha ya kodi, upangaji bei hovyo kwa bidhaa za Tanzania, biashara haramu kati ya Tanzania na nchi za nje au makampuni ya kimataifa halafu wananchi wakubali kupumbazwa na bidhaa za milioni chache zinatolewa na viongozi wa umma walioshindwa kurekebisha hali hii”, Mwisho wa kunukuu. Msingi wa msimamo huu unaweza kurejewa kwa ukamilifu hapa: http://mnyika.blogspot.com/2010/03/natangaza-rasmi-dhamira-ya-kugombea.html
Mosi; kusikiliza na kuwakilisha wananchi, Pili; kuisimamia na kuiwajibisha serikali na viongozi wake, Tatu; kushiriki katika kutunga sheria, Nne; kuhamasisha upatikanaji wa huduma.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya wabunge wetu hawaweki kipaumbele katika majukumu ya kwanza matatu ambayo ndio msingi wa ubunge wenyewe. Matokeo yake ni matakwa ya wananchi kutokuwakilishwa kikamilifu, ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mikataba mibovu; uwepo wa sheria dhaifu na kutetereka kwa utawala wa sheria na mifumo ya haki masuala ambayo yanakwaza jitihada za maendeleo za wananchi binafsi za taifa kwa ujumla.
Wabunge wengi wanawaza kwamba jukumu kubwa la mbunge ni kutoa bidhaa na huduma kwa wananchi; wakiacha taifa katika lindi la umasikini na kufanya sehemu ya wananchi kujenga mazoea ya kutegemea hisani toka kwa viongozi wa umma na wafadhili wao.
Mwaka 2005 pamoja na majukumu hayo makuu matatu, nilizungumzia suala la mfuko wa maendeleo ya jimbo. Lakini si katika mwelekeo wa mfuko wa sasa uliopitishwa kuwa sheria. Kwa hiyo, wakati nikiunga mkono jukumu la mbunge kuhamasisha maendeleo na kushiriki kwenye shughuli za kijamii, siamini katika mazoea na mfumo wowote unaomfanya mbunge kuwa “mtoa bidhaa na huduma” (mithili ya ATM) kwani unarutubisha ufisadi wa kisiasa na kuhatarisha mwelekeo mzima wa utawala bora. Kama ambavyo siamini pia katika siasa chafu za rushwa, uongo na aina nyingine ya upofu wa kimaadili katika kampeni na uongozi kwa ujumla.
Haiwezekani wakati ambapo makisio yanaonyesha kwamba zaidi ya trilioni mbili (sawa na milioni milioni mbili) zinapotea kila mwaka kupitia misamaha ya kodi, upangaji bei hovyo kwa bidhaa za Tanzania, biashara haramu kati ya Tanzania na nchi za nje au makampuni ya kimataifa halafu wananchi wakubali kupumbazwa na bidhaa za milioni chache zinatolewa na viongozi wa umma walioshindwa kurekebisha hali hii”, Mwisho wa kunukuu. Msingi wa msimamo huu unaweza kurejewa kwa ukamilifu hapa: http://mnyika.blogspot.com/2010/03/natangaza-rasmi-dhamira-ya-kugombea.html
Hivyo, ufanisi wa ubunge wangu upimwe kwa kuzingatia msimamo huo
ambao niliwaeleza wananchi wakati wa uchaguzi hivyo nilichaguliwa ikifahamika
wazi kuwa huo ndio wajibu ambao nitautekeleza katika kipindi cha miaka
mitano.
Bado naendelea kuamini kwamba jimbo la Ubungo na taifa kwa ujumla
tutapiga hatua ya haraka zaidi ya maendeleo kupitia mabadiliko katika mifumo
yetu ya mgawanyo wa rasilimali na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na pia
kwa kuweka mazingira bora ya kisera, kisheria na kiutendaji wa sekta
binafsi.
Tuliyoyafanya mpaka sasa ni sehemu tu katika mahitaji makubwa ya
maendeleo kutokana na pengo la miaka 50 ukilinganisha na fursa ambazo taifa letu
linazo; hata hivyo naamini miaka mitatu iliyobaki itafanya miaka mitano ya
kuisimamia Serikali iliyopo madarakani hivi sasa pamoja na udhaifu wote
uliokuwepo kuleta tofauti katika maendeleo majimboni. Ni katika muktadha huo
wakati mwingine tunazimika kuwakilisha na kuwasilisha matakwa ya wananchi namna
hii: http://www.youtube.com/watch?v=ES4OMOD_xME tukiamini
kwamba watawala wenye dhamana kwa sasa ya kukusanya kodi watasikiliza na
kuzingatia vipaumbele vya maendeleo vya wananchi.
Aidha, baada ya kazi mkutano wa nane wa bunge naomba kutumia fursa
mjadala utakaofuatia taarifa hii kupata maoni yenu kuhusu masuala ninayopaswa
kuyapa kipaumbele katika kuwawakilisha na kuwatumikia jimboni katika kipindi cha
mwezi Septemba mpaka Oktoba 2012 kabla ya kuanza kwa mkutano wa tisa wa bunge na
pia kuhusu maandalizi ya mwaka 2013. Kero nyingi zinazoendelea kuwepo kwa sasa
ni neema iliyojificha (blessing in disguise) ili tuendelee kuunganisha nguvu ya
umma kuendeleza wimbi la mabadiliko.
Narudia tena kuwakumbusha kuwa nguvu ile ile tuliyoitumia kwenye
kutafuta kura na kulinda kura ndio naiomba toka kwenu katika hatua hii ya
kufanya kazi za kuwezesha maendeleo kwa kutimiza wajibu kila mmoja wetu kwa
nafasi yake, kuisimamia serikali na kuunganisha rasilimali za wadau
wengine;
Maslahi ya Umma Kwanza.
Nimeandika taarifa hii leo tarehe 21 Agosti 2012 siku ya kumbukumbu
ya kuzaliwa kwangu.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
Jimboni-Ubungo
No comments:
Post a Comment