KATIBU Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ), Dk. Willibrod Slaa, amesema kuwa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kinachukiwa na wananchi kutokana na kuendelea kujitetea kwa
kutumia sababu zilizotumiwa na wapigania uhuru wa Tanganyika kujikomboa katika
mikono ya wakoloni.
Akizungumza katika mikutano
ya hadhara kwenye vijiji mbalimbali vya kata za Ngerengere na Makambarai, Dk.
Slaa alisema serikali ya CCM imeshindwa kutengeneza fursa ya wananchi kujiletea
maendeleo yao licha ya kuwa katika nchi yenye rasilimali nyingi.
“Mwalimu Nyerere pamoja na
wapigania uhuru wengine wa Tanganyika hawakumkataa mkoloni kwa sababu ya rangi,
dini wala hali zao isipokuwa waliwakataa kwa vile walishindwa kuwaondolea watu
umaskini, ujinga na maradhi ambayo yanaendelea kutuandama kila wakati,”
alisema.
Alisema kuwa hayati Mwalimu
Nyerere alifikia malengo kwa kuonesha njia ya kupita, hivyo waliomfuatia
walikuwa na wajibu wa kuhakikisha njia hiyo inapitika lakini serikali ya CCM
imeamua kuziba njia hiyo.
Huku akisoma takwimu za
maendeleo katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, linaloongozwa na Dk. Lucy
Nkya (CCM), Dk. Slaa alisema kuwa hakuna sababu ya kuendelea kukivumilia chama
hicho kwa sababu ya kufanana kwa rangi na badala yake wananchi wanapaswa
kuchukua hatua ya kukipumzisha.
“Kila mmoja hapa amesikia
takwimu nilizosoma, tena zinatokana na vitabu vya serikali yenu hii mliyoichagua
na kuiweka madarakani, mlichagua rais wa CCM, mbunge wa CCM, Diwani wa CCM,
mwenyekiti wa kijiji na serikali ya kijiji ya CCM, sasa nawasomea hapa ufisadi
unaofaywa mnaanza kusikitika,” alisema.
Alisema ni aibu miaka 50
baada ya Uhuru kusikia Watanzania wakizungumzia upungufu wa madawati wakati nchi
nyingine zikiwa zinashindana kwenda kuangalia uwezekano wa kufanya utafiti
utakaozisaidia nchi zao.
No comments:
Post a Comment