POLISI
WAHAHA KUFICHA UKWELI, WATOA DAU LA MIL. 5/-
WASHTAKIWA wawili
waliompora askari polisi bunduki wakiwa chini ya ulinzi katika mahakama ya mkoa
wa Arusha na kutoroka kusikojulikana, katika mazingira ya kutatanisha imebainika
kuwa ni wale wanaokabiliwa na tuhuma ya mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Usa River, Msafiri
Mbwambo.
Washtakiwa hao Samweli
Mtinange maarufu kama Samu na Mohamed Shaban Limu walitoroka juzi majira ya saa
7:30 mchana wakati wakitolewa kwenye chumba cha mahabusu mahakamani wakipelekwa
kwenye karandinga la polisi kwa ajili kurudishwa rumande kwenye gereza la mkoa,
Kisongo.
Kamanda wa polisi mkoani
hapa, Liberatus Sabas, alithibitisha kutoroka kwa washtakiwa hao wanaokabiliwa
na kesi hiyo ya mauaji namba 184/2012, lakini akakanusha kuporwa bunduki na
silaha zaidi ya 30 kwa askari polisi aliyekuwa akiwalinda.
Tukio hilo limezua hofu
kubwa na kuzusha tuhuma kuwa limepangwa kiufundi na baadhi ya watu, kwa nia
mahsusi za kisiasa hasa ikizingatiwa kutokea kwa tukio jingine baya la mauaji ya
mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, mkoani Iringa
mwanzoni mwa mwezi uliopita.
Wasiwasi huo umekuja
kutokana na mazingira ya tukio hilo, ambalo wadadisi wa mambo wanatia shaka juu
ya kutokuwepo kwa mikakati imara iliyosukwa kufanikisha utorokaji
huo.
Kurugenzi ya Ulinzi na
Usalama ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imedai kupokea kwa
mshtuko na tahadhari kubwa, kitendo cha watuhumiwa wawili wa mauaji hayo,
kutoroka mbele ya askari polisi wenye silaha, baada ya kumnyang’anya bunduki
mmoja wa askari waliokuwa lindo kwenye eneo la mahakama ya wilaya.
Aidha kurugenzi pia
imepokea kwa tahadhari kubwa taarifa kuwa Kamanda wa Polisi (RPC), mkoa wa
Arusha, Liberatus Sabas, pamoja na kukiri kuwa waliokimbia mbele ya polisi kwa
kumnyang’anya askari silaha ni watuhumiwa wa mauaji ya Mbwambo, aligoma kutaja
jina la askari aliyenyang’anywa bunduki na hata majina ya wenzake waliokuwa
lindo hapo mahakamani.
Katika taarifa kwa vyombo
vya habari Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Rwakatale,
alisema tukio hilo sasa limekifanya chama hicho kianze kuweka mkazo kwenye
kuunganisha ‘nukta’ katika matukio ya namna hii na limezidi kudhihirisha pasi na
shaka yoyote umuhimu wa kuundwa kwa chombo huru cha uchunguzi wa mauaji yenye
utata, yanayohusishwa na siasa, mojawapo likiwa ni tukio la mauaji ya
Mbwambo.
Rwakatale amelitaka Jeshi
la Polisi kutoa maelezo ya kutosha yatakayoendana na uwajibikaji, unaopaswa
kufuatiwa na hatua za kisheria, ili kuweza kujinasua kwenye kashfa hii ya juzi
Arusha, ambapo sasa inatafsiriwa kuwa jeshi hilo limehusika kufanya ‘mchezo’
mwingine kwa nia ama ya kutaka kuficha mtandao wa mauaji hasa ya kisiasa au
kuficha ushahidi muhimu wa masuala ambayo ama yamebainika kwenye mahojiano au
ambayo yangebainika mahakamani, ikizingatiwa kuwa baadhi ya watuhumiwa wa kesi
hiyo ni viongozi wa CCM.
“Kitendo cha RPC Sabas
kukanusha askari wake kunyang’anywa bunduki, ambayo baadaye iliokotwa ikiwa
imetelekezwa, ni dalili za mwendelezo wa tabia ya jeshi hilo, kupitia maofisa
wake waandamizi, kujitokeza kuficha ukweli na kufanya propaganda, kwa kila tukio
ambalo jeshi hilo linapaswa kuwajibika kwa makosa linayofanya”
“Itakumbukwa pia katika
barua ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman Mbowe kwenda kwa Rais, chama
kilimtaka Rais kuunda Tume ya Kijaji/ Kimahakama ya uchunguzi wa vifo
vilivyotokea katika mikusanyiko, mikutano, maandamano au mazingira ya kisiasa
yaliyohusisha CHADEMA. Vifo hivi ni vile vilivyotokea Arusha (05/01/2011),
Igunga (Novemba 2011), Arumeru Mashariki (Aprili 2012), Iramba (Julai 14, 2012),
Morogoro (27/08/2012) na Iringa (02/09/2012),” imesema taarifa
hiyo.
CHADEMA imesema kuendelea
kutokea kwa masuala yenye utata katika usalama kumeonyesha kuwa serikali ya CCM
inazidi kukomaza mfumo wa kulindana na kutaka kuficha masuala fulani fulani,
hasa katika matendo ya mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi, chini ya Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Hali ambayo inatia shaka ni hatma ya ulinzi na
usalama wa raia na mali zao.
“Hatuoni mantiki ya
kigugumizi cha serikali ya CCM na viongozi wake, kushindwa kuzungumzia
utendekaji wa haki na uwajibikaji kama moja ya misingi muhimu sana ya tunu ya
amani.
Masuala haya yakitekelezwa
inavyotakiwa, hata kazi ya ulinzi na usalama kwa raia na mali zao, itakuwa
rahisi kwa sababu itakuwa ni wajibu wa jamii nzima. Kinyume na hapo, kwa
kufumbia macho vitendo vya wazi vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu,
ikiwemo isiyoweza kuthaminishwa na kitu chochote, haki ya kuishi, inazidi
kujipotezea uhalali wa kutawala.
CHADEMA imeendeleaa
kusisitiza kutaka uwajibikaji wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel
Nchimbi, IGP Saidi Mwema, Kamanda wa Operesheni Maalum wa Jeshi la Polisi, Paul
Chagonja, RPC wa Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile na RPC wa mkoa wa Iringa,
Michael Kamuhanda, kutokana na mauaji yaliyotokea mkoani Morogoro na Iringa, kwa
wao wenyewe kujiuzulu au kufukuzwa kazi na Rais ili kupisha uchunguzi
huru.
“Wakati Kurugenzi
ikisisitiza msimamo wa chama wa kuitaka serikali iwakamate na kuwafungulia kesi
ya mauaji, Kamanda wa FFU Mkoa wa Morogoro (kwa mauaji ya Ally Zona) na RPC
Kamuhanda na askari wote wanaoonekana kwenye picha wakimsulubu marehemu Daudi
Mwangosi kabla hajalipuliwa kwa bomu la polisi na kufa, inapenda kusisitiza kuwa
Jeshi la Polisi linawajibu wa kuhakikisha watuhumiwa wa mauaji ya Mbwambo
waliotoroka, Samwel Mtinange na Mohamed Limu, wanapatikana huku hatua
zinazostahili juu ya tukio hilo la utorokaji zikichukuliwa kwa wahusika wote,”
wamesema.
Mbali na waliotoroka,
washtakiwa wanaoendelea kushikiliwa kuhusiana na mauaji ya Mbwambo ambaye
aliuawa kikatili kwa kukatwa kichwa na kitu chenye ncha kali shingoni kubaki
wanne wakiwemo wenyeviti wa serikali za vitongoji wanaotokana na Chama cha
Mapinduzi (CCM), Davis Mkumba (Kisambaramajengo) na Mathias Nathan (Magadini)
ambapo washtakiwa wengine ni Saidi Florianna Swalihi na Yohana.
Aidha hatua ya Kamanda
Sabas kukanusha taarifa kuwa watuhumiwa hao wakati wakitoroka walifanikiwa
kumnyang’anya bunduki mmoja wa askari waliokuwa wakilinda, mashuhuda wa tukio
hilo ambao hawakuwa tayari majina yao kutajwa magazetini walilieleza Tanzania
Daima kuwa watuhumiwa hao walimnyang’anya silaha aina ya SMG mmoja wa askari
polisi aliyekuwa akiwalinda jambo lililozua hofu kubwa miongoni mwa baadhi ya
watumishi wa mahakamani ambao baadhi waliamua kujifungia ndani ya vyumba vya
mahakama wakihofia mahabusu huyo kuwafyatulia risasi.
Mashuhuda hao waliendelea
kudai kuwa mmoja wa mahabusu hao alikuwa wa kwanza kutoka kwenye chumba cha
mahabusu na alipomkaribia askari huyo ambaye jina wala cheo chake hakijafahamika
alimvamia na kumpora silaha hiyo inayodaiwa kuwa na risasi 30 na kuruka uzio
mrefu wa mahakama hiyo.
Jeshi la Polisi limewaomba
wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa
washtakiwa hao ambapo limetangaza zawadi nono ya shilingi milioni tano kwa
wananchi watakaofanikisha kukamatwa ikiwa ni shilingi milioni 2.5 kwa kila
mtuhumiwa.
Tanzania
Daima
No comments:
Post a Comment